Bungei akataa kuzungumzia tukio la mshukiwa wa mauaji kutoroka seli
NA SAMMY KIMATU
KAMANDA wa Polisi katika Kaunti ya Nairobi Adamson Bungei mnamo Ijumaa alikataa kuzungumzia kisa cha mshukiwa wa mauaji ya mwanamke nchini Marekani aliyetoroka seli za kituo cha polisi cha Muthaiga.
Adam Kevin Kinyanjui Kang’ethe alitoweka katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga alimokuwa akizuiliwa baada ya ubalozi wa Marekani kuomba Kenya isaidie kumsafirisha hadi nchini humo kushtakiwa kwa kumuua mpenzi wake na kisha kuutupa mwili wake kwenye uwanja wa ndege na kutorokea nchini.
Lakini Bw Bungei akiwahutubia wanahabari wakati wa hafla ya Maombi ya Makamanda katika Kaunti ya Nairobi iliyofanyika katika uga wa Pavillion katika mtaa wa South C, eneobunge la Starehe, alikwepa swali kumhusu mshukiwa huyo.
Soma Pia: Mwanamume aliyefaa kupelekwa Marekani kushtakiwa atoroka seli
Badala yake, Bw Bungei alisema maafisa wake wako chonjo kila wakati na kuongeza kwamba usalama katika jiji la Nairobi umeimarishwa.
“Sitaki kuzungumzia kisa cha Muthaiga lakini ninawahakikishia wakazi wa Nairobi kwamba usalama wao pamoja na mali zao ni salama chini ya ulinzi wa polisi. Jukumu letu ni kudumisha amani na kuhudumia raia kama ilivyo kikatiba na kisheria kwa muda wa saa 24,” Bw Bungei akasema.
Alikuwa ameandamana na Naibu Kamishna Mkuu wa Polisi Douglas Kanja.
Katika hafla hiyo ya kufana, makamanda hao walifika katika uga wa Pavilion saa kumi na moja asubuhi kabla ya kushiriki nyimbo na ibada na sifa, zilizoongozwa na kanisa la Universal Church of the Lord.
Wageni wote walikaribisha kwenye mkutano na mkuu wa polisi katika Kaunti ndogo ya Lang’ata Monicah Wambui.
Kadhalika, mahubiri yaliongozwa na Askofu Mkuu katika Kanisa la Christian Foundation Fellowship Harrison Ng’ang’a huku jukumu la kutoa shukrani na kuongoza hafla ya kiamsha kinywa likitwikwa Kamanda wa Polisi eneo la Cental Doris Kemrey.
Baada ya kukamilika kwa sherehe, Bw Bungei aliongoza maafisa wake katika shughuli muhimu ya uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miche ya miti katika uwanja huo.