Habari za Kaunti

Hofu ndege wakivamia mashamba ya mpunga Mwea

Na GEORGE MUNENE October 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKULIMA wa mpunga Mwea wanahofu ya kupata hasara baada kundi kubwa la ndege kuvamia mashamba katika mradi wa unyunyuziaji maji mashamba wa Mwea, Kaunti ya Kirinyaga.

Kuna hofu kuwa ndege hao maarufu kama Quelea wanaweza kumaliza mpunga shambani iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Maeneo ambayo yameathiriwa sana ni Thiba, Nguka, Wamumu, Mathangauta, Marura, Mutithi na Kimbimbi ambapo mpunga hupandwa kwa wingi.

“Tumeanza kushuhudia ndege wengi juma lililopita na hali ni mbaya,” mmoja wa wakulima Bw Robinson Kibicho akasema.

Wakulima wamekuwa wakipambana nao bila mafanikio na sasa imebidi wawaajiri watu wa kuwinga ndege kwa malipo ya Sh300 kwa siku kwa ekari moja.

Shamba la mpunga Mwea, Kaunti ya Kirinyaga. Picha|Labaan Shabaan

Kila mkulima ana shamba ekari nne katika mradi wa maelfu ya ekari za mashamba.

“Tunalipa pesa nyingi sana kufukuza ndege ambao wamevamia mashamba yetu,” mkulima mwingine alisema.

“Iwapo ndege hawa hawatadhibitiwa, huenda kukawa na uhaba mkubwa wa mchele nchini,” Bw kibicho akaongeza.

Wakulima sasa wanaomba serikali ya Kaunti ya Kirinyaga iingilie kati kuokoa mazao yao.“Kilimo kimegatuliwa, kwa hivyo serikali ya kaunti inafaa kuwanyunyizia ndege dawa wasiharibu mimea yetu,” alisema Bw Kaberi Muriuki akikiri kuwa ni serikali pekee inaweza kuwasaidia.

“Tunaomba serikali ifanye upesi na kutusaidia,” alisema Bw Kibicho akieleza kuwa wanategemea mpunga kujiendeleza kimaisha.

Mradi huu ndio mkubwa zaidi nchini na huzalisha asilimia 80 ya mchele Kenya.

Kwa sasa, taifa hili hukuza tani 130, 000 kila mwaka, kiasi ambacho hakitoshi kulisha wananchi.

Mkulima aonyesha mmea wa mpunga shambani Mwea. Picha|Labaan Shabaan

Imetfasiriwa na Labaan Shabaan