Kawira ataka MCA kufungwa jela kwa kupanga kumtimua mamlakani
GAVANA wa Meru Kawira Mwangaza anataka Mahakama Kuu kuwahukumu maafisa wawili wa bunge la kaunti na MCA aliyeteuliwa kwa madai walidharau mahakama, akisema walipuuza maagizo ya korti kwa kukusudia kumtimua kwa mara ya tano.
Anataka Spika Ayub Bundi, Karani wa bunge hilo Jacob Kirari na MCA Zipporah Kinya wahukumiwe kifungo cha miezi sita jela na kutozwa faini kwa jukumu walilotekeleza katika kuondoa hoja hiyo.
Katika ombi lililoidhinishwa kuwa la dharura, Bi Mwangaza alibainisha kuwa licha ya maagizo hayo, Bi Kinya tayari amewasilisha hoja ya tano ya kumuondoa mamlakani ambayo inatarajiwa kujadiliwa Agosti 8, 2024.
Gavana huyo aliitaka mahakama kuwazuia madiwani kujadili, kuzingatia na kupitisha hoja hiyo mpya akisema atapata hasara isiyoweza kurekebishwa ikiwa mahakama haitaingilia kati haraka.
Kupitia kwa mawakili Elias Mutuma na Ashaba Mark, gavana huyo anasema kukosa kuwazuia madiwani kujadili hoja ya Julai 31 kutafanya ombi la awali kutokuwa na maana.
“Washtakiwa wanaendeleza uovu uliokusudiwa kuepushwa na maagizo ya awali ya mahakama hii kwa hivyo wana hatia ya kudharau mahakama.
“Wamekaidi na wanataka kuona hoja ya kuondolewa mamlakani kupitia mchakato wa Bunge la Kaunti bila kuzingatia sheria na haswa maagizo ya Mahakama hii Tukufu,” akasema.
Punde baada ya mahakama kutoa maagizo hayo, gavana huyo anadai kuwa madiwani wanaounga mkono ombi la kuondolewa mamlakani kwake walinukuliwa wakiikashifu mahakama kwa kuitupilia mbali.
Alisema madiwani waliandika barua kali ya “kumpinga jaji, kuidhalilisha mahakama na kufanyia mzaha maagizo ya mahakama hiyo.”
Bi Mwangaza aliitaka mahakama kuwaadhibu watatu hao ili kuhakikisha madiwani “wanatii sheria na kuheshimu hadhi ya mahakama.”
“Katika dhihaka na dharau ya wazi ya kesi za korti walalamishi walifichua katika barua iliyotajwa kuwa hawatashiriki katika kesi yoyote mbele ya mahakama hii tukufu.
“Ninakumbuka kwamba mwaka jana wakati mahakama ilitoa amri sawa katika hoja ya kwanza ya kunitimua, washtakiwa walitaka kutishia mahakama kwa kutoa barua kama hiyo,” alisema katika hati ya kiapo.
Bi Mwangaza aliitaka mahakama iamue kuwa bunge hilo “lina hatia ya kutumia mamlaka yake kinyume cha sheria, kupita kiasi na kwa njia ya matusi” kwa kuwasilisha hoja tano za kumuondoa mamlakani katika kipindi cha miaka miwili.
Anashutumu bunge hilo kwa kuwa na upendeleo, na anasema kwamba ikiwa hoja haitasimamishwa, haki zake za kusikilizwa kwa haki kama ilivyohakikishwa chini ya Kifungu cha 50(1) cha Katiba ya Kenya zitakiukwa.
Gavana huyo anasema mahakama ilikuwa imetoa maagizo ya dhidi ya bunge hilo, ikiwakataza madiwani kujadili hoja ya kumuondoa mamlakani ambayo iliwasilishwa Julai 31, 2024.
Anasema kuwa maagizo yaliyotolewa Julai 24, 2024 yalisitisha mchakato wa kumtimua ofisini hadi uamuzi utakapotolewa kuhusu masuala yaliyoibuliwa na waliopinga mchakato huo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Meru Linus Phogon Kassan alikuwa amesema kwamba uamuzi wa Agosti 20, 2024 ungeshughulikia madai ya kughushi saini za baadhi ya madiwani kwenye karatasi zinazounga mkono hoja ya kumuondoa mamlakani Gavana Mwangaza.