KDF yabomoa jengo hatari kwa ustadi
KIKOSI cha pamoja kikiongozwa na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) Jumatano, Aprili 9, 2025 kilibomoa jengo la ghorofa 11 katika mtaa wa Fayaz Estate, Mombasa, kwa mlipuko uliodhibitiwa, na hivyo kumaliza siku kadhaa za taharuki eneo hilo.
Jengo hilo, lililokuwa Kilifi Coner kwenye Barabara ya Abdel Nasser, lilibomolewa saa sita na dakika 55 mchana baada ya kutangazwa kukosa muundo imara kuonekana kuwa hatari.
Operesheni hiyo ilifanyika kufuatia hofu kuongezeka tangu Aprili 2, 2025, wakati jengo hilo lilipoanza kuzama.
Ubomoaji huo wa kudhibitiwa ulihitimisha juhudi za dharura zilizoanzishwa na vikosi vya kijeshi, polisi, maafisa wa kaunti na wataalamu wa kiufundi.
KDF walitumwa rasmi jijini humo kupitia tangazo la gazeti la serikali lililotolewa na Waziri wa Ulinzi, Roselinda Soipan Tuya, Aprili 7, 2025.
Tangazo hilo, chini ya Kifungu 241(3)(b) cha Katiba pamoja na Sheria ya KDF, liliwaruhusu wanajeshi kusaidia mamlaka za kiraia kushughulikia dharura hiyo.
Kwa mujibu wa mamlaka, jengo hilo lilikuwa tishio kwa majirani na wakazi wa mtaa wa Fayaz.
Hivyo, Serikali ya Kaunti ya Mombasa na Wizara ya Usalama wa Ndani ziliamuru watu wote ndani ya mzunguko wa kilomita 1.2 kuondoka mara moja.
Maafisa wa kaunti walitumia mwishoni mwa wiki kutoa onyo mara kwa mara, wakihimiza wakazi kuondoka eneo hilo kabla ya ubomoaji.
Kikosi cha pamoja kutoka KDF, polisi, vitengo vya dharura vya kaunti na wahandisi kilifunga eneo hilo na kusimamia zoezi la uokoaji na ubomoaji kwa utaratibu.
Wakati huo huo, katika maeneo mengine ya jiji, athari za tukio hilo zilionekana kwa biashara na huduma za umma.
Upande wa magharibi mwa Mombasa, waendeshaji wa matatu waliripoti biashara duni.
“Wafanyabiashara wengi kutoka mjini wanaonunua bidhaa Kongowea walibaki nyumbani. Safari zilikuwa chache sana,” alisema Peter Mwadime, kondakta kutoka Jomvu.
Katika Kituo cha Afya cha Mlaleo, kulishuhudiwa ongezeko la wagonjwa.
“Mara nyingi watu hupendelea Hospitali ya Rufaa ya Pwani lakini kwa sababu ya kufungwa kwa muda wagonjwa wengi walikuja hapa,” alisema afisa mmoja aliyeomba tusitaje jina lake.
Jengo hilo, tangu lilipoanza kuzama wiki moja iliyopita, lilikuwa chanzo cha hofu kwa wakazi na wafanyabiashara mtaa wa Fayaz.
Mnamo Jumanne, eneo hilo lilikuwa chini ya ulinzi mkali huku wanajeshi na polisi wakilifunga kabisa, kuzuia shughuli zozote.
Kulikuwa na hali ya sintofahamu mjini Mombasa mapema Jumatano, baada ya shughuli nyingi kutatizika kufuatia maandalizi ya ubomoaji wa jumba hilo.
Kuanzia saa kumi alfajiri, steji ya matatu kuanzia Bombolulu hadi Lights zilifurika wasafiri waliokuwa wakiharakisha kabla ya kufungwa kwa barabara hiyo kuanzia Daraja la Nyali hadi Soko la Mackinnon, hali iliyotarajiwa kudumu kwa angalau saa nne.
Tangazo la kufungwa kwa barabara lilitolewa jioni ya Jumanne na Serikali ya Kaunti ya Mombasa, ikisisitiza kuwa hatua hiyo ilikuwa kwa usalama wa wakazi wakati wa ubomoaji wa jengo la ghorofa 11.