Kilele cha ukatili watu 9 wa familia moja wakiuawa kwa kuchomwa wakilala
WAKAZI wa kijiji cha Upanda, eneo la Sigomre, Ugunja Jumatano waliamkia habari za kusikitisha za kuangamizwa kwa watu 9 wa familia moja- mwanaume, mke wake, na watoto wao saba kwenye moto.
Polisi wanashuku kwamba tukio hilo lina uhusiano na mzozo wa muda mrefu wa ardhi unaohusisha familia hiyo.
Kulingana na maelezo ya polisi, wanne kati ya waathiriwa waliteketea vibaya hadi kutotambulika, huku miili ya wengine ikipatikana katika mabaki ya nyumba iliyoungua.
Kwa mujibu wa polisi, miongoni mwa waliouawa ni mwanafunzi wa shule ya upili aliyekuwa akijiandaa kwa mtihani wa kitaifa, na mtoto mchanga wa miezi sita, jambo lililozua maswali zaidi kuhusu ukatili huo.
Polisi walisema kwamba mwanaume mwenye umri wa miaka 45, ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa familia, alikuwa akizozania ardhi na familia nyingine.
Polisi waliongeza kuwa suala hilo tayari lilikuwa limeamuliwa mahakamani.
Miili ya marehemu ilipelekwa hadi mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Siaya kwa uchunguzi wa maiti huku polisi wakiendelea na uchunguzi wao huku picha zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zikionyesha nyumba hiyo ikiwa imeharibiwa kabisa mali ya binafsi ikiwa majivu.
Jana, polisi walithibitisha kuwa mshukiwa mmoja alikamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Mshukiwa ni mwanamke aliyehusika katika mzozo wa umiliki wa ardhi walimoishi marehemu.
Mkuu wa DCI katika eneo la Nyanza, George Mutonya, alisema mshukiwa atafunguliwa mashtaka ya mauaji na kuchoma moto huku msako dhidi ya washukiwa wengine ukiendelea.
‘Tunawasaka washukiwa wengine kuhusiana na mauaji haya,. Tunatumaini kuwapata hivi karibuni,’ alisema.
Mshukiwa alipatikana na mtungi uliokuwa na kile ambacho polisi wanaamini ni petroli iliyotumika katika shambulio hilo. Mashahidi waliambia polisi kuwa wahalifu hao walifika kwa gari, wakatekeleza uhalifu huo, kisha wakatoroka.
Walifunga milango ya nyumba hiyo kutoka nje kabla ya kuwasha moto.
Agizo la mahakama la kuifukuza familia hiyo kutoka kwenye ardhi lilikuwa tayari limetolewa.
Polisi walisema kuwa kufukuzwa kwa familia hiyo kulipangwa kufanyika Alhamisi.
Kwa hasira, wakazi walienda nyumbani kwa mshukiwa na kuchoma nyumba
Polisi wamesema wameimarisha usalama katika eneo hilo ili kuzuia machafuko zaidi kwa taharuki ingali imetanda.
Visa vya uchomaji moto na mauaji vinaripotiwa kuongezeka katika eneo hilo.
Wiki iliyopita, watu watano wa familia moja waliuawa katika tukio sawia huko Masimba, Kaunti ya Kisii.
Wahalifu pia walichoma nyumba sita katika tukio hilo ambalo lilihusishwa na kisa cha awali cha mauaji. Katika kisa cha Kisii, waathiriwa waliuawa kikatili kabla ya miili yao kuchomwa moto.