Habari za Kaunti

Lalama za wanawake Lamu wanaume kulemaza jitihada za upanzi wa miti


WANAWAKE wanaojishughulisha na uhifadhi wa mazingira, Kaunti ya Lamu wamewafokea wenzao wa jinsia ya kiume kwa kile wanachodai ni kuendeleza uharibifu wa misitu, hasa ile ya mikoko.

Aidha, wanawake hao wanalalamikia kuachiwa jukumu la upanzi wa miti na urejesho wa hadhi ya mazingira.

Kaunti ya Lamu inasifika kwa kuwa na asilimia kubwa ya msitu wa mikoko ipatikanayo nchini Kenya ambayo ni karibu 65.

Tangu jadi, jamii ya Lamu imesifika sana kwa kuendeleza masuala yanayofungamana na uhifadhi na uendelezaji wa mikoko, hulka ambayo imekuwa ikirithiwa kutoka kizazi hadi kizazi.

Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali, baadhi ya akina mama wanaojituma kuhifadhi mazingira waliwalaumu wanaume kwa kujikita sana katika kukata na kuuza mikoko ilhali mzigo wa upanzi na urejesho wa miti hiyo kwenye maeneo ilikovunwa na kumalizwa ukiachiwa wanawake.

Fatma Omar, mwanaharakati wa mazingira kutoka Mtangawanda, Lamu Mashariki, alisema hawana raha kuona wanaume wakifurahia mtaji unaotokana na wao kuikata mikoko ilhali wakipuuza majukumu muhimu ya upanzi.

Bi Omar alipongeza wanawake wa Lamu kwa kuweka kipaumbele upanzi, uhifadhi na uendelezaji wa msitu wa mikoko licha ya kukosa ushirikiano kutoka kwa wanaume wengi.

“Kitega uchumi cha jadi kwa wanaume wetu ni uvuvi wa samaki, kukata na kuuza mikoko. Hilo ndilo lilitufanya sisi wanawake wa Lamu kujituma sana kwenye upanzi wa mikoko ili biashara yenyewe ya mikoko na pia uvuvi usikosekane. Yaani mikoko na samaki inahusiana pakubwa,” akasema Bi Omar.

Akaongeza, “Hatuna budi ila kupanda na kuhifadhi mikoko ili kuzuia hawa waume wetu kukosa kazi, iwe ni uvuvi au ukataji mikoko. Mikoko hutoa mazingira mazuri ya samaki kuzaana. Ila hatufurahii tukiona wanaume wakijisahau. Wanavuna mikoko bila kufikiria kupanda mingine.”

Kauli yake iliungwa mkono na Bi Nana Abdalla aliyesisitiza haja ya kila jinsia, iwe ni wanaume au wanawake, kushirikiana kuendeleza uhifadhi wa mikoko.

“Mikoko na samaki ni muhimu kwetu sote. Kweli wanaume wetu tunawasaidia wasikose kazi kwa kuhakikisha mikoko inahifadhiwa na kuendelezwa, ila isiwe sababu ya wao kupuuza kabisa hili suala la upanzi na uhifadhi wa mikoko na mazingira yetu kwa jumla. Wasijikite tu kukata mikoko au kuvua samaki bila kujukumikia suala zima la uhifadhi,” akasema Bi Abdalla.

Sehemu ambazo ni tajika sana kutokana na mikoko kuharibiwa Lamu miaka ya nyuma ni Kililana, Njia ya Ndovu, Manda Tita, Kibodo, Ndau, Kipungani na Kitangani.

Juhudi mbalimbali zimekuwa zikiendelezwa na makundi ya akina mama, mashirika ya kijamii, yale ya kibinafsi, taasisi za serikali, ikiwemo shirika la huduma za misitu nchini (KFS) miongoni mwa wengine.

Mbali na kupatia watu riziki kupitia uvunaji na uuzaji na pia kuwa mazao bora ya samaki, mikoko pia husafisha hewa kwenye mazingira, hasa yale ya Pwani, hivyo kuyafanya maeneo hayo kuwa bora ya kuishi.