Magenge ya vijana wa Gen Z yanavyohangaisha wakazi Kitale
GENGE moja la vijana barobaro limegeuka kero kwa wakazi mjini Kitale kwa kutekeleza wizi wa mabavu wakitumia silaha hatari.
Matineja hao, ambao wanaishi maisha ya anasa, wanaogopwa katika mitaa mbalimbali ya makazi ambako wao hujificha wanapofanya mashambulio ya kulipiza kisasi dhidi ya majirani wanaowaripoti kwa maafisa wa usalama.
Baadhi yao hujificha katika biashara ya boda boda lakini baadaye huwaandama wakazi kwa kuiba na hata kuharibu mali yao nyakati za usiku.
Hata hivyo, baadhi ya wahalifu hao wa umri mdogo wameishia kuuawa na polisi, magenge pinzani au wakazi wenyewe.
Mitaa ya Tuwan na Matisi viungani mwa mji wa Kitale ndio inakisiwa kuwa maficho ya vijana hao wahalifu.
Kulingana na takwimu kutoka kwa Idara ya Watoto, kuna zaidi ya watoto 3,000 waliotelekezwa katika Kaunti ya Trans Nzoia, wengi wao wakishukiwa kuhusika katika uhalifu.
Mkurugenzi wa Idara hiyo katika Kaunti ya Trans Nzoia Jonnah Maingi amewalaumu wazazi kwa kutowajibika na kuwaacha watoto wao kujiingiza katika uhalifu na vitendo vingine vya utovu wa maadili.
“Tuna wazazi ambao hawajui yale ambayo matineja wao wanafanya au mahala ambapo wao huenda kila siku kabla ya kurejea nyumbani. Tuna shida ya visa vya matineja kupata ujauzito na maovu mengine kutokana na ongezeko la idadi ya watoto waliotelekezwa,” Bw Maingi akaeleza.
Jane Gitonga, mkazi wa eneo la Mitume Booster, alisimulia aliyopitia mikononi mwa magenge hayo ya wahalifu matineja akirejea nyumbani kutoka shughuli za kibiashara mjini Kitale.
“Wavulana hao wenye silaha butu walinisimamisha nikielekea nyumbani na kutisha kunibaka na kuniua. Niliwapa Sh40,000 pesa za biashara ili wasinidhuru,” akaeleza masaibu yake wakati wa mkutano wa kiusalama ulioongozwa na Kamishna wa Kaunti Gideon Oyugi mnamo Agosti 27, 2024.
Maafisa wa utawala wakiwemo wanachama wa Nyumba Kumi na wazee wa mitaa walifichua kuwa chimbuko la visa vya utovu wa usalama ni matumizi ya pombe haramu na dawa za kulevya katika eneo hilo.
“Hamna ushirikiano kati ya machifu na polisi katika eneo letu. Sababu ni kwamba machifu wanapowakamata wahalifu, maafisa wa polisi huwaachilia huru baada ya kupewa hongo,” akasema Samuel Mwaura.