Mshukiwa wa mauaji ya mwanaharakati wa LGBTQ Chiloba apatikana na hatia
MAHAKAMA Kuu jijini Eldoret imempata na hatia mshukiwa mkuu wa mauaji ya mwanaharakati wa LGBT.
Mahakama ilimpata Jackton Odhiambo, mpiga picha wa kujitegemea na hatia ya mauaji ya Edwin Kiptoo, almaarufu Chiloba.
Mnamo Jumatano Jaji Reuben Nyakundi alitoa uamuzi wake mwaka mmoja tu baada ya mauaji hayo ya kutisha, ambayo yalizua hisia mseto kote duniani.
Akitoa uamuzi wake, Jaji Reuben Nyakundi alisema mshukiwa huyo alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu ambaye alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Eldoret kabla ya mwili wake uliokuwa umeharibika kupatikana siku sita baadaye ukiwa umetupwa kando ya barabara katika Kaunti ya Uasin Gishu.
Jaji Reuben Nyakundi alisema atahukumu mshtakiwa mnamo Desemba 16, 2024.
Bw Odhimabo alishtakiwa kwa kumuua Chiloba aliyekuwa akisomea shahada ya Mavazi, Mitindo na Ubunifu katika chuo kikuu cha Eldoret kaunti ya Uasin Gishu.
Alikana kumuua Chiloba ambaye anasemekana kuwa rafikiye wa chanda na pete kati ya Desemba 31, 2022 na Januari 3, 2023, katika nyumba za makazi za Noble Breeze Apartments eneo la Chebisaas, kaunti ndogo ya Moiben.
Mwili wa marehemu uligunduliwa kwenye sanduku la chuma kando ya barabara ya Kipkenyo-Kaptinga katika Kaunti Ndogo ya Kapseret mnamo Januari 3,2023.
Jaji alisema kuwa Odhiambo alimdhulumu Chiloba licha ya kuwa alimtaja kuwa rafiki yake wa karibu kabla ya kupanga njama ya kifo chake ambacho alisema kilikuwa cha kikatili katika nyumba ambayo walikuwa wakiishi pamoja.
Marehemu alikuwa na alama mikononi mwake ambazo ziliashiria kuwa alijaribu kujikinga akishambuliwa.
Jaji alitilia mkazo kuwa ushahidi uliowasilsihwa mahakamani ulithibitisha kuwa Odhiambo alimuua Chiloba.