Mtihani ulivyosimamishwa kwa muda baada ya gesi hatari kuzagaa shuleni Makande
WATAHINIWA wa mtihani wa kitaifa wa sekondari, KCSE, katika shule ya upili ya Makande Girls jijini Mombasa, walilazimika kuhamia shule jirani kukamilisha mtihani wa Kiswahili, baada ya gesi iliyodaiwa kuwa hatari kuzagaa hewani na kusababisha wanafunzi watano kukimbizwa hospitalini.
Tukio hilo, lililosababisha hali ya mshikemshike katika shule hiyo, lilithibitishwa na Afisa Mkuu wa dharura za mikasa ya Moto, Bw Ibrahim Basar.
“Tulipokea simu kutoka kwa afisa mkuu wa polisi wa jijini Maxwell Agoro, kuhusiana na hali hiyo. Tulielezwa kuwa kulikuwa na hewa hatari iliyokuwa ikinuka katika maeneo ya shule hiyo,” akasema.
Kikosi cha taasisi mbalimbali kikiongozwa na idara ya kuzima moto Mombasa, kilifika pamoja na timu ya Mamlaka ya Bandari nchini ya kushughulikia vitu Hatari (HAZMAT), Shirika la Msalaba Mwekundu na ambulensi za idara ya dharura za kiafya kaunti hiyo.
Wazo lao la kwanza lilikuwa kutambua aina ya gesi iliyokuwa ikinuka.
“Tumefahamishwa kuwa wanafunzi watano wamekimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Pwani kwa matibabu. Tutazuia eneo hili na kuchunguza wanaohusika,” akasema Bw Basafar.
Kwa mujibu wa maafisa, viwango vya hewa hiyo vilikuwa vimepungua kwa kiasi na ilikuwa imeondoa hali ya hatari.
Licha ya hayo, mamlaka mbalimbali zilifika kuchunguza ilikotokea gesi hiyo, ikiwemo idara ya upelelezi ya makosa ya jinai (DCI), mamlaka ya kudhibiti mafuta ya Petroli (EPRA) zikishirikiana na idara ya kushughulikia dharura za moto.
Mkurugenzi wa Elimu kaunti Ndogo ya Mvita Bw Ali Aden, alieleza kuwa gesi hiyo haikutoka kwenye shule yenyewe.
“Wanafunzi watano wamekimbizwa hospitalini huku wengine 84 wakipelekwa shule ya Wavulana ya Wavulana ya Makupa kuandika mtihani wa Kiswahili Lugha,” akasema Bw Aden.
Shule hiyo iko karibu sana na eneo maalum la viwanda eneo la Mombasa.