Habari za Kaunti

Mwangaza wa Mwangaza wazima korti ikiidhinisha kutimuliwa kwake kama gavana wa Meru   

Na RICHARD MUNGUTI March 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu imeidhinisha kutimuliwa kwa Askofu  Kawira Mwangaza kama gavana wa Meru.

Jaji Bahati Mwamuye, akitoa uamuzi wake Ijumaa, Machi 14, 2025, alithibitisha uamuzi wa Seneti, ambao uliidhinisha kubanduliwa kwa Bi Mwangaza na Bunge la Kaunti ya Meru kwa misingi ya utovu wa nidhamu, matumizi mabaya ya mamlaka, na ukiukaji mkubwa wa Katiba.

Katika uamuzi wake, Jaji Mwamuye alibainisha kuwa Seneti ilifuata Katiba ipasavyo wakati wa mchakato wa kumng’oa Mwangaza. Alikataa hoja ya Mwangaza kwamba mchakato huo ulikumbwa na vurugu, akisema kwamba alishindwa kuthibitisha madai yake.

Kwa uamuzi huu, muhula wa Mwangaza kama gavana umekatizwa rasmi, baada ya kufika mahakamani mara kadhaa akijaribu kuokoa wadhifa wake.

Hata hivyo, Mwangaza bado anaweza kukata rufaa katika mahakama za juu na kujaribu kuokoa taaluma yake ya kisiasa.

Kufuatia kuondolewa kwake, Naibu Gavana wa Meru, Mchungaji Isaac Mutuma M’Ethingia, anatarajiwa kuchukua hatamu za uongozi kama Gavana wa Meru kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa Mwangaza.

Hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Kenya ya 2010, ambayo inahakikisha hakuna ombwe la uongozi katika wadhifa muhimu kama wa gavana, ili kuhakikisha uendelevu wa uongozi wa kaunti.