Naibu wa Nabii Owour ashtakiwa kwa kumchafulia jina mshirika kwenye Whatsapp ya kanisa
KIONGOZI wa vijana kitengo cha uinjilisti katika kanisa la Nabii David Owour Mjini Eldoret, amemshtaki naibu wa mhubiri huyo kwa madai ya kumpaka tope.
Mlalamishi anayehusishwa na Kanisa la Repentance and Holiness – linalomilikiwa na Nabii Owour, anasema pasta huyo alimchafulia jina kwenye kundi la Whatsapp la kanisa hilo.
Bw Simon Aluchio, muumini wa muda mrefu, kwenye kesi aliyowasilisha katika mahakama ya Eldoret, anamlaumu naibu askofu Jackson Barno, katika kile anahoji kama ‘machapisho yake’ yalichochea kutorokwa na msichana aliyetaka kufunga ndoa naye.
Askofu Barno anatuhumiwa kumkashifu mshirika huyo kupitia kundi la Whatsapp la kanisa la Owour linalojulikana kama Overseers UG madhabahu kuu.
Mlalamishi anasema mchungaji huyo alichapisha nyenzo za kuudhi ambazo zinafanya aonekane kama mtu “mchafu na mwovu”, na vilevile kusababisha asimamishwe kazi katika kanisa hilo.
Kupitia stakbadhi zake mahakamani, alisema nia ya ujumbe huo kwenye mtandao wa WhatsApp wa kanisa hilo ni kumharibia mipango ya kumtafuta mchumba ndani ya kanisa na kufanya harusi.
Alidai kwamba chapisho hilo litawaogopesha wapenzi watarajiwa.
Aluchio ambaye pia ni mhudumu aliyeidhinishwa katika Mahakama Kuu ya Kenya, anadokeza kuwa askofu wake alichapisha maneno hayo ya kuudhi mnamo Juni 5, 2024 mwendo wa saa kumi na moja (11:03) za jioni kupitia nambari yake ya simu ya rununu.
Alisema chapisho hilo lilipakiwa bila idhini yake.
Kulingana naye, kitendo cha askofu huyo kimemharibia nafasi ya kupata mpenzi aliyeokoka kanisani ambapo amekuwa akiabudu kwa zaidi ya miongo miwili.
Bw Aluchio anamtaka pasta Barno kuwajibika kwa hatua yake kupitia mchakato wa kisheria kwa kumchafulia jina.
Akijibu madai hayo, mtumishi wa Mungu alitja hatua ya Bw Aluchio kufika mahakamani kama kejeli kwa kanisa na kusema kuwa ingekuwa bora iwapo angetumia baraza la wazee kutafuta upatanisho badala ya kukimbia kortini.
Hata hivyo, aksofu huyo alisema yuko tayari kukabiliana na kesi hiyo kisheria.