Habari za Kaunti

Sanamu ya Faith Kipyegon iliyokera Wakenya yaondolewa usiku wa giza

Na WINNIE ONYANDO August 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI ya Kaunti ya Uasin Gishu, Jumatano, Agosti 14, 2024 ililazimika kuondoa sanamu mbovu iliyoundwa kuwakilisha mwanariadha maarufu duniani Faith Chepngetich Kipyegon usiku baada ya sanamu hiyo kukosolewa vikali na Wakenya kwenye mitandao ya kijamii.

Hii ni baada ya picha ya sanamu yenye sura ya kuchanika ya mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mita 1,500 aliye pia bingwa wa Olimpiki kupeperushwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Sanamu hiyo iliyowekwa kwenye mzunguko karibu na Hospitali ya Mediheal, mjini Eldoret, ilionyesha mwanariadha huyo wa kike akiwa katika pozi ya kukimbia, akiwa amevalia fulana iliyo na bendera ya Kenya na kushika kitu kilichoonekana kama upanga.

Wakenya kwenye mitandao ya kijamii walikisia haraka kwamba sanamu hiyo ilikusudiwa kuwakilisha Faith, aliye bingwa mara tatu wa Olimpiki katika mbio hizo.

Baadhi ya Wakenya walikerwa na ‘kinyago’ hicho wakisema hakifanani hata kiduchu na Kipyegon.

Hisia za Wakenya zilionekana kuwagusa maafisa wa serikali ya Uasin Gishu na kufikia asubuhi ya leo Agosti 15, sanamu hiyo ilikuwa imeondolewa usiku baada ya wimbi la ukosoaji kutoka kwa Wakenya.

Sanamu ilikuwa imesimikwa kando ya barabara kuu ya mji huo kabla ya tukio muhimu la kuukweza mji wa Eldoret kuwa jiji.

Sherehe hiyo inayofanyika leo Alhamisi, itashuhudia Rais William Ruto akiwasilisha mkataba wa hatua hiyo ya kukweza mji hadhi kwa Gavana wa Uasin Gishu, Jonathan Bii.

Hafla hiyo, iliyokuwa imepangwa kufanyika Agosti 8, iliahirishwa hadi Agosti 15 baada ya mashauriano na serikali ya kitaifa.

Rais Ruto pia alikuwa akiwapokea wanariadha waliopeperusha bendera ya Kenya kwenye Olimpiki ya Paris.