Habari za Kaunti

Seneti yaanika Kaunti ya Kwale kwa kutokamilisha miradi

Na SIAGO CECE May 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Kwale, Fatuma Achani amekosolewa vikali baada ya maseneta kubaini miradi kadhaa ya kaunti ambayo haijakamilika au haifanyi kazi ipasavyo.

Kamati ya Seneti ya Uwekezaji wa Umma na Hazina Maalum ilipotembelea Kaunti ya Kwale, iligundua kuwa baadhi ya miradi inayofadhiliwa na walipa ushuru haijakamilika, licha ya sifa nyingi kutoka kwa serikali ya kaunti.

Katika Hospitali ya Rufaa ya Msambweni, kamati hiyo ilieleza wasiwasi wake kuhusu wagonjwa kuchelewa kuhudumiwa.

Kompyuta moja tu ndiyo ilikuwa ikitumika kusajili wagonjwa, hali iliyowafanya wengi kusubiri kwa muda wa zaidi ya saa tatu kabla ya kupata huduma.

“Tunahitaji huduma za afya zifanywe kwa njia ya kielektroniki ili kuondoa msongamano wa wagonjwa katika hospitali hii ya pekee ya rufaa,” alisema mwenyekiti wa kamati hiyo,” Seneta Geoffrey Osotsi.

Maseneta walikutana kwanza na Gavana Achani, ambapo alitangaza kuwa miradi ya bomba la maji la kilomita 14 na kituo cha mabasi cha Diani ilikuwa imekamilika.

Lakini walipofika eneo la Tiwi, waliona kipande kifupi tu cha bomba hilo limechimbwa. “Tulimpongeza gavana mapema sana. Hili shimo haliwezi kuitwa kilomita 14. Maji bado yanapotea kwa kiwango kikubwa,” alisema Seneta Osotsi.

Katika Kituo cha Mabasi cha Diani, walikuta sehemu kubwa imefunikwa na mahema ya wachuuzi, hakuna ofisi za tiketi, wala huduma ya maji na umeme. Badala ya mabasi, walikuta wachuuzi wakiuza mboga.

“Hii inaonekana kama soko la wazi, si kituo cha mabasi. Ikiwa kaunti inaita hiki ‘kimekamilika’, basi kuna mambo mengine mengi wanayopamba kwa maneno,” alisema Seneta William Kisang.

Katibu wa Kaunti, Bi Sylvia Chidodo, alitetea miradi hiyo akisema bado inahitaji marekebisho kidogo.
Maseneta pia walitoa wito kwa serikali kuu kuharakisha kutoa fedha zinazodaiwa kwa kaunti ili kusaidia huduma kwa wananchi na kukamilisha miradi.

Seneta Maalum, Bw Raphael Chimera, alikiri kuwa mfumo wa SHA haujafanya kazi vizuri kutokana na uhaba wa kompyuta, hali inayosababisha msongamano na ucheleweshaji wa huduma.

Alimtaka Waziri wa Afya, Bw Adan Duale kuhakikisha fedha za kaunti zinatolewa kwa wakati ili kuboresha huduma katika hospitali za umma.