Serikali yaweka ua wa umeme kulinda Msitu wa Mau
SERIKALI imeweka ua wa umeme ili kulinda msitu wa Mau dhidi ya uharibifu katika eneobunge la Narok Kusini, Kaunti ya Narok.
Ua huo unazingira kilomita 70 kati ya kilomita 400 ambazo zilikuwa zinalengwa.
Kwa mujibu wa Waziri wa Misitu Gitonga Mugambi, hatua hiyo imechukuliwa kuzuia uharibifu na pia kuongeza upanzi wa miti ili msitu huo uendelee kuwa na miti mingi.
Bw Mugambi alisema juhudi za kulinda msitu huu zinatekelezwa na serikali kwa ushirikiano na wafadhili kutoka mashirika na washikadau.
Pia alisema ua kuwekwa msituni humo kutasaidia kupunguza mizozo kati ya binadamu na wanyamapori. Vile vile, inalenga kuhakikisha kuwa miti mingi inapandwa ili kuzuia athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa miaka mingi, kumekuwa na uhasama kati ya wakulima kwenye mashamba ya kibinafsi na usimamizi wa misitu. Hii ni licha ya kuwa serikali imewapa wakulima hao vyeti vya kumiliki ardhi, baadhi vikiwa vimefutiliwa mbali.
“Tupo kwenye awamu ambapo tumeshaanza kuongea na jamii za hapa ili waelewe manufaa ya mpango huu wa kuzingira msitu kwa ua na kupanda miti,” akasema Bw Mugambi.
Katibu huyo alisema jamii zinazoishi karibu na msitu wa Mau zinastahili kuelewa umuhimu wa kutunza Mau ambayo ni chemchemi ya maji kwa mito inayopeleka maji yake Ziwa Viktoria.
Baadhi ya mito hiyo ni Mara Mara, Sondu Miriu, Nyangores, Amalo na Chemosit. Msitu wa Mau upo kwenye kaunti za Nakuru, Narok, Bomet, Kericho na Baringo na pia ni nyumbani kwa wanyamapori na aina mbalimbali ya ndege.
Kwa miaka mingi, uharibifu mkubwa umekuwa ukiendelea kwenye msitu wa Mau huku serikali ikiraiwa iendeleze juhudi za kuuokoa wakati ambapo utawala wa Rais William Ruto nao umeweka malengo ya kupandwa kwa miti bilioni 15 nchini kufikia 2030.