Habari za Kaunti

Shule pabaya kaunti ikikosa kutekeleza ahadi ya kuwalipia wanafunzi karo

Na MANASE OTSIALO September 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WALIMU wakuu kutoka Kaunti ya Mandera wamemshutumu Gavana Mohamed Adan Khalif wakisema alitoa ahadi za uongo kupitia mpango aliouanzisha wa Elimu kwa Wote, unaoelekea kuporomoka.

Mpango huo ulishirikisha utawala wa kaunti kuwalipia wanafunzi wote wa sekondari asilimia 60 ya karo kwa wanafunzi kwenye shule za malazi na asilimia 70 kwa wale wanaosomea shule za kutwa.

Mandera ni kati ya kaunti ambazo zina viwango vya juu vya umaskini.

Walimu wakuu wanalalamika kuwa kaunti imekuwa ikiwahadaa na mpango huo unalemaza shughuli zao shuleni.

“Pesa zimekuwa zikichelewa kutumwa au wakati mwingine hazitumwi kabisa na pia hakuna orodha maalum ya wanafunzi ambao wananufaika,” akasema Ali Hassan Ali, Mwenyekiti wa Muungano wa Walimu wa Shule za Upili (KESSHA) tawi la Mandera.

Kwa mujibu wa KESSHA  wanasiasa wameuteka mpango huo na wanautumia kupiga siasa za kujinufaisha ilhali shule hazipati pesa zenyewe.

“Tutakutana na gavana na maafisa wake baada ya karo za muhula wa kwanza na wa pili kulipwa. Iwapo hatutapata pesa hizo kati ya Septemba 13 hadi Septemba 16, tutawatuma wanafunzi wote nyumbani,” akasema Mwekahazina wa Kessha Mahat Ibrahim.

“Tunasisitiza kuwa kaunti lazima iwe na maelewano rasmi kuhusiana na mpango huo. Maelewano hayo yanastahili kuwa kati ya Wizara ya Elimu, wabunge wa hapa na Kessha,” akaongeza.

Alipofikiwa, Mkurugenzi wa Elimu Ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa, Adan Roble alisema kuwa wanafunzi wengi hawajalipiwa karo na kaunti jinsi ilivyoahidi.

“Kuna hili utata huu kuhusu karo na tumetoa wito kwa pande zinazohusika kuelewana la sivyo nitamwaandikia katibu wa wizara ya elimu ili hatua  ichukuliwe,” akasema Bw Roble.

Afisa huyo alisema shule zimekuwa zikipokea mgao kutoka kwa serikali japo ile kaunti iliahidi kulipa bado haijafikia shule husika.

Mandera ina zaidi ya shule 67 za umma ambazo zina wanafunzi 23,000.

Walimu wakuu nao walilalamika wamelemewa kulipa bili za umeme, maji huku wazazi nao wakikosa kulipa chochote wakisema kaunti ilishatwaa jukumu la kuwalipia hela.

Waziri wa Elimu wa kaunti Bashir Alio alisema kucheleweshwa  kwa fedha hizo ni kutokana na walimu wakuu kukosa kuwasilisha data inayohitajika.

Bw Alio alisema ni shule 15 kati ya 68 ndizo zimewasilisha data zao na mchakato wa kuhakiki data hiyo ulikuwa ukiendelea.

“Pia serikali kuu haijakuwa ikitoa mgao kwa wakati na shule zinastahili kuwasilisha data yao kufikia Septemba 14 ili mchakato wa kuihakiki ukamilike,” akasema Bw Alio.