Spika azima vikao vya bunge la kaunti baada ya madiwani kuingiana mangumi
SPIKA wa Bunge la Machakos, Anne Kiusya, Jumanne, Aprili 8, 2025 alisitisha vikao vya Bunge kwa muda usiojulikana baada ya siku ya kizaazaa ambapo diwani wa wadi ya Matungulu Magharibi, Raphael Nzau, alijeruhiwa makundi mawili pinzani ya wawakilishi wadi yalipopigana huku Seneta Agnes Kavindu, akimtaka Gavana wa kaunti hiyo, Wavinya Ndeti, kuwasiliana na Spika wa Bunge kutatua mvutano wa madiwani unaoendelea.
“Bi Ndeti anapaswa kuongoza upande wa serikali ya kaunti kuketi na Bunge la Kaunti ili kumaliza mvutano unaoendelea miongoni mwa Madiwani kwa njia ya amani. Mvutano huu umeongezeka na unahatarisha utoaji huduma kwa wananchi,” alisema Bi Kavindu Jumanne baada ya Bi Kiusya kusitisha vikao vya Bunge kwa muda usiojulikana kwa madai ya ukosefu wa usalama.
“Vikao vya madiwani wote na vya Kamati za Bunge la Kaunti vimesimamishwa hadi wakati ambapo usalama wa Spika, madiwani, na wafanyakazi utahakikishwa.
“Safari rasmi za madiwani za ndani na za nje ya nchi, pia zimesimamishwa,” alisema Bi Kiusya katika taarifa baada ya madiwani kuharibu samani walipokuwa wakirushiana mangumi katika siku yao ya kwanza baada ya mapumziko.
Shida ilianza baada ya kundi moja la madiwani kupinga jaribio la uongozi wa Bunge kuanzisha hoja ya kuondolewa kwa Kiongozi wa Wachache wa Machakos, Judas Ndawa.
Bw Ndawa ni miongoni mwa wawakilishi wadi wa Machakos ambao wamekuwa wakishinikiza kuondolewa kwa Bi Kiusya.
“Bw Nzau alijeruhiwa baada ya ghasia kutokea tulipopinga jaribio la Spika kupenyeza pendekezo la kutilia shaka katika shughuli za Bunge. Madiwani wanasisitiza hawako tayari kujadili chochote chini uongozi wa Bi Kiusya. Hatutakubali,” alisema Naibu Spika wa Machakos na Mbunge wa Ekalakala, Stephen Mwanthi, akizungumza na waandishi wa habari baada ya ghasia zilizotawala kikao cha Jumanne.
Bi Kiusya alijifungia ofisini mwake kwa siku nzima.
Kizaazaa katika bunge la kaunti ya Machakos ni mabadiliko mapya katika mzozo unaochacha kati ya makundi mawili ya madiwani wa kaunti ya Machakos.
Kundi moja linataka kumuondoa Bi Kiusya huku la pili likitaka kumuondoa Gavana wa Machakos, Wavinya Ndeti.
Bw Mwanthi ni kiongozi wa madiwani ambao wamewasilisha pendekezo la kumwondoa Bi Kiusya. Wanamshutumu kwa kutokuwa na uwezo na mfisadi.
Amekanusha vikali madai kwamba alitumia pesa za umma kumpeleka binti yake, June Kilonzo, Ulaya na Falme za Kiarabu miaka miwili iliyopita.
Hii ni mojawapo ya sababu nane zilizomo katika pendekezo la kumuondoa Bi Kiusya ambalo Kiongozi wa Wengi wa Machakos, Nicholas Nzioka, amewasilisha katika Bunge la kaunti.
Madiwani walioungana na Gavana Ndeti, pia wanamshutumu Bi Kiusya kwa kushindwa kutambua Judah Wewa, mshirika wa Bi Ndeti ambaye anamezea mate uongozi katika Bunge la Kaunti.
Walikuwa wameonya kuwa asijitokeze bungeni baada ya Mahakama Kuu kuzuia mpango wa kumuondoa ofisini hadi kesi iliyowasilishwa na Bi Kiusya itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Jaji Rodah Rutto aliahirisha kusikilizwa kwa kesi ya kumuondoa spika huyo hadi Aprili 30.
Sehemu ya madiwani wanaopinga kuondolewa kwa Bi Kiusya wameahidi kumuondoa Bi Ndeti ambaye wanamshutumu kwa kupanga kumtimua Bi Kiusya.