Habari za Kaunti

SULTANI MWENYEWE! Wafuasi wasifia Joho kuteuliwa waziri, Jumwa akila hu!

Na ANTHONY KITIMO Na SIAGO CECE July 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

PUNDE tu baada ya Rais William Ruto kutangaza uteuzi wa mawaziri huku akimteua Hassan Ali Joho kama Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, wakazi wa Mombasa walijitokeza barabarani wakisherehekea uteuzi huo.

Mamia ya wakazi wa Mombasa waliimba nyimbo za kupongeza Rais Ruto huku wakiapa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kusitisha maandamano Pwani.

“Twashukuru Rais kwa kuanzisha serikali ya muungano na sisi watu wa Mombasa tuko kwa serikali na tutammuunga mkono Bw Ruto. Tuko na imani simba wetu Bw Joho atakuelekeza vilivyo,” alisema Bi Jumwa Karisa, mkazi wa majengo.

Vijana kutoka vitongoji mbalimbali mjini Mombasa walikusanyika na kufanya maandamano ya amani wakisema wizara hiyo inawahusu moja kwa moja kwani sehemu kubwa ya Pwani ni bahari.

“Tunamatumaini sekta ya uvuvi na madini itaboreshwa wakati huu kwani kazi ya naibu kiongozi wa ODM ambaye pia alikuwa Gavana wa Mombasa imekuwa ikionekana,” alisema mmoja wa waandamanaji.

Kurudi kwa Bw Joho kama Waziri kutasismua siasa za Pwani ambazo zilionekana zikididimia kufuatia kutoka kwake kama gavana.

Bw Joho amekuwa na umaarufu katika siasa na tangu kutoka kwake hakujatokea mwanasiasa kutoshea viatu vyake kwani ana umaarufu na ushawishi wake wa pesa.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir, alijumuika na wakazi kumpongeza Bw Joho akimtaja kuwa kiongozi mwenye maoni.

“Kwa juhudi zako za kuhudumia umma na uongozi mzuri ,sina hofu utaweza kuongoza wizara hiyo,” alisema Gavana Nassir.

Hapo jana, Rais Ruto alitangaza Bw Joho na aliyekuwa Gavana wa Kwale Salim Mvurya kama mawaziri wateule huku wakisubiri uchunguzi wa bunge kabla ya kupewa nafasi hiyo ya uongozi.

Bw Mvurya ambaye alikuwa akishikilia wizara ya madini na uchumi wa baharini aliteuliwa kwa wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda huku wakazi wa Kwale nao wakijawa na furaha kufuatiwa kuteuliwa kwake tena.

Hata hivyo, Bw Mvurya alisema kuwa yuko tayari kufika kikao cha bunge ambacho kitafanya uchunguzi na kutathmini uongozi wake katika wizara hiyo.

“Namshukuru sana Rais Ruto na niko tayari kupigwa msasa kwenye kikao cha bunge,” Bw Mvurya alisema.

Kwa upande wake, Gavana wa Kwale Fatuma Achani amempongeza Rais Ruto kwa kumteua Bw Mvurya kama waziri kwani ana ujuzi na uongozi bora.

“Ningependa kumshukuru Rais Ruto kwa kumteua kwa wizara ya Uwekezaji, Biashara, na Viwanda. Pia ningependa kumshukuru kwa kumteua Bw Joho,” alisema Bi Achani.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ilikuwa ushindi mkubwa kwa eneo la Pwani ambapo magavana wa awali wameteuliwa kwa wizara muhimu kwenye baraza la mawaziri.