Tahadhari ya mafuriko mijini mvua ikianza
SERIKALI ya Kaunti ya Kajiado imetoa tahadhari ya mafuriko, ikionya wakazi wanaoishi kwenye maeneo ya mito kuepuka vifo na uharibifu wa mali mvua za masika zinapoanza Aprili.
Kulingana na utabiri wa hivi majuzi wa hali ya hewa kutoka Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya, uliowiana na utabiri wa jadi uliofanywa na wazee mnamo Februari, Kajiado ni miongoni mwa kaunti zinazotarajiwa kupokea mvua nyingi kuliko viwango vya kawaida kati ya Machi na Mei.
Wakati wa mkutano wa dharura kati ya usimamizi wa manispaa, usimamizi wa miji na wananchi siku ya Alhamisi mjini Kitengela, serikali ya kaunti ilionya kuhusu idadi kubwa ya familia zinazoishi kwenye ardhi ya mito katika miji midogo kama Ong’ata Rongai, Kiserian, Ngong, Kitengela, na Kajiado.
“Waliovamia maeneo ya mito tunataka wahame mara moja kabla hatujawafurusha kwa nguvu,” alisema James Saloni, Mwenyekiti wa Manispaa ya Kajiado.
“Ni aidha mafuriko yawafukuze au sisi tuwafukuze ili tuwaokoe kabla ya msimu wa mvua kuanza, wanachezea kifo,” aliongeza.
Watu wanaoishi maeneo ya bondeni wamehimizwa kuhamia maeneo ya juu na kuepuka kuvuka vijito vilivyojaa maji ili kuepuka kusombwa na mafuriko.
Chama cha Muungano wa Wakazi wa Kaunti ya Kajiado (K-CARA), ambacho ni mwavuli wa vyama mbalimbali vya wakazi wa manispaa, kupitia Mwenyekiti wake Parsimei Gitau, kimeelezea wasiwasi kuhusu ongezeko kubwa la unyakuzi wa ardhi ya umma, ikiwemo maeneo ya mito.
Bw Gitau alisema kuwa mwenendo huu wa kutisha umeathiri upangaji bora wa miji katika kaunti nzima.
“Tumeona watu wakijenga nyumba za makazi kando ya mito. Wajue kwamba huwezi kubadilisha mkondo wa mto.
Ni wakati mwafaka wa kuwaondoa ili kuepusha maafa,” alisema Bw Gitau.
Aidha, alikemea unyakuzi wa ardhi ya huduma za umma unaoendelea katika Kaunti ya Kajiado, hasa mijini.
Mji wa Kitengela umewahi kukumbwa na athari kubwa za mafuriko.
Mei 2024, mvua kubwa isiyo ya kawaida iliyosababisha mafuriko ilisababisha vifo vya watu wawili, uharibifu mkubwa wa mali, na familia takriban 300 kupoteza makazi yao kutokana na mafuriko .
Maeneo ya New Valley, Balozi Road, na Tropicana Road yaliyoko kando ya Mto Ilkeek-lemedung’i, unaofahamika kama New Valley River, yaliathirika pakubwa.