Taharuki Ledama akiandaa mkutano Kajiado na kuzima mwenyeji wake
KUNDI la vijana lilivuruga mkutano wa kisiasa uliojaa taharuki, uliopangwa na Seneta wa Narok, Ledama Ole Kina, katika Sajiloni, Kajiado ya Kati huku Seneta wa Kajiado, Samuel Seki, akizuiwa kuhudhuria.
Seneta Ledama aliwasili kwa helikopta na alikuwa karibu kuanza kuhutubia umati, lakini muda mfupi baadaye, Seneta wa Kajiado, Samuel Seki, naye aliwasili kwa helikopta pamoja na Mbunge wa Kajiado Kusini, Samuel Parashina, na wagombeaji wa nyadhifa mbalimbali za kisiasa.
Ingawa Seki aliweza kufika kwenye hema kuu na karibu kuingia katika sehemu ya watu mashuhuri, kikosi cha maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami vilivyo kilimzuia.
Taharuki ilizuka huku baadhi ya wananchi wakikimbia kutoka kwenye mahema.
Mkutano huo, ambao haukuhudhuriwa na viongozi wengine wengi wa Kaunti ya Kajiado isipokuwa Mbunge wa Kajiado Mashariki, Kakuta Mai Mai, uliwaleta pamoja maelfu ya watu waliolishwa nyama ya ng’ombe 50 waliochinjwa kwa hafla hiyo.
Mkutano huo tata uliandaliwa kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na umoja wa kisiasa na uwezeshaji wa vikundi vya wanawake na vijana Kajiado.
Akiwa amejawa na hasira, Seneta Ledama aliwashutumu wapinzani wake wa kisiasa akisema kuwa mkutano huo ulikuwa wa kuleta umoja kuinua jamii ya Wamaasai kutoka kwa umasikini.