UGATUZI WA AIBU: Hospitali gizani Taita Taveta baada ya stima kukatwa, jenereta kukosa mafuta
HOSPITALI ya Wesu iliyoko katika kaunti ndogo ya Wundanyi, Kaunti ya Taita Taveta, imetumbukia gizani baada ya Kampuni ya Umeme (KPLC) kukata stima kutokana na deni la Sh1.7 milioni.
Kampuni hiyo ilikata umeme mnamo Jumatatu jioni, na hivyo kuathiri huduma muhimu za matibabu, na kuwaacha wagonjwa na wahudumu wa afya katika hali ya wasiwasi.
Jumatatu usiku wagonjwa walilazimika kutumia mishumaa katika wodi zao, huku huduma muhimu za matibabu zikisitishwa, na hivyo kuhatarisha maisha ya waliohitaji huduma za dharura.
Kukosekana kwa umeme kumeathiri huduma muhimu kama vile upasuaji wa dharura, X-ray, maabara, vitengo vya watoto wachanga na chumba cha kuhifadhia maiti.
Ingawa hali hiyo ingeokolewa na jenereta ya dharura ya hospitali hiyo, jenereta hiyo ilishindwa kufanya kazi kutokana na ukosefu wa mafuta.
Duru za kuaminika zilidokeza Taifa Leo kuwa kituo cha mafuta kilichokuwa kikiuzia hospitali hiyo kilikataa kuleta mafuta zaidi hadi deni linalodaiwa kaunti hiyo lilipwe.
Hali hiyo ilisababisha wagonjwa kukosa huduma muhimu za matibabu, na kusababisha madhara makubwa kwa afya zao.
Serikali ya kaunti ilinunua jenereta hilo kwa Sh4.9 milioni mnamo Agosti mwaka huu ili kukabiliana na ukosefu wa umeme wa mara kwa mara katika hospitali hiyo na kuhakikisha shughuli zinaendelea bila matatizo.
Hata hivyo, ukosefu wa mafuta kwa sasa umefanya jenereta hilo kushindwa kufanya kazi kama ilivyokusudiwa, na hivyo kuzidisha tatizo hilo.
Kulingana na mdokezi huyo, ambaye aliomba jina lake libanwe kwa kutoruhusiwa kutoa habari kwa vyombo vya habari, alionya kuwa hospitali hiyo inaweza kupata hasara kubwa ikiwa umeme hautarejeshwa mara moja.
“Kuna madawa, na sampuli za wagonjwa zinazohitaji kuhifadhiwa kwenye friji na ziko hatarini kuharibika ikiwa hali hii itaendelea. Chumba cha kuhifadhia maiti pia kimeathirika sana,” alisema.
Usimamizi wa hospitali hiyo bado haujatoa habari zozote kuhusu hali hiyo. Daktari mkuu wa kutuo hicho, Dkt Rukia Mkamburi hakujibu simu na jumbe zetu.
Hata hivyo, serikali ya kaunti hiyo imewahakikishia wagonjwa na wakazi kuwa suala hilo linashughulikiwa.
Afisa Mkuu wa Idara ya Afya Violet Mkamburi alisema kuwa mazungumzo na Kampuni ya KPLC yanaendelea ili kurejesha umeme hospitalini huku Idara ya Fedha ikishughulikia kulipa deni hilo leo (Jumanne).
“Idara ya Fedha inashughulikia fedha za kulipa deni hilo. Ni kweli hospitali ni kituo muhimu, na ndio maana tunaenda mbio kuhakikisha umeme unarejeshwa haraka iwezekanavyo,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa changamoto za kifedha zinazokabili serikali ya kaunti zimezidisha hali hiyo.
Hivi majuzi, Kenya Power ilikata umeme katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Moi, Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Mwatate, na Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Taveta kutokana na madeni ya mamilioni ya pesa.
Vilevile, soko la Voi na afisi ya gavana pia zilikatiwa umeme, jambo ambalo liliathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zao.