Habari za Kaunti

Wafanyabiashara wapata hasara pepo la moto likurudi Gikomba

Na HAPPINESS LOLPISIA April 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HAPPINESS LOLPISIA

WAFANYABIASHARA katika soko la Gikomba, Nairobi, Jumatatu, Machi 31, 2025 walipata hasara tena baada ya moto mkubwa kuharibu vibanda na mali yao.

Moto huo uliozuka mwendo wa saa tisa usiku uliendelea kwa saa kadhaa kabla ya kudhibitiwa na wazima moto.

Janga hilo la moto limeamsha tena hofu kuhusu milipuko ya mara kwa mara ya moto katika soko la Gikomba, jambo ambalo limeendelea kutatiza wafanyabiashara, na kuwaacha wakihangaika kuanzisha biashara zao upya.

Wafanyabiashara hao wameilaumu serikali ya kaunti kwa uzembe na kushindwa kuweka mikakati kuzuia majanga ya moto ili kulinda biashara zao.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, aliposhika madaraka mwaka wa 2022, aliahidi kushughulikia tatizo la moto na kulinda wafanyabiashara wa Gikomba.

Akikiri kuwa migogoro ya ardhi ni mojawapo ya sababu kuu za milipuko ya moto, aliahidi kuimarisha soko hilo kama ardhi ya umma na kuchukua hatua dhidi ya wavamizi wa ardhi.

Soko la Gikomba, ambalo ndilo soko kubwa zaidi la wazi jijini Nairobi, limekumbwa na milipuko mingi ya moto kwa miaka mingi, mara nyingi ikisababisha hasara kubwa.

Juni 25, 2020, moto mkubwa uliteketeza sehemu ya kuuzia nafaka na nguo za mitumba, ukaharibu mali ya thamani isiyojulikana.

Mwaka 2021, zaidi ya wafanyabiashara 900 walishtaki serikali ya Kaunti ya Nairobi, wakidai fidia ya Sh20 bilioni kwa hasara waliyopata kutokana na mikasa ya moto ya mara kwa mara.

Mnamo Oktoba 15, 2022, sehemu ya soko hilo iliteketea, hali iliyosababisha mwito wa hatua za haraka kutoka kwa serikali.

Mnamo Septemba 2023, wafanyabiashara walipoteza bidhaa za thamani ya zaidi ya Sh2 milioni kwenye mkasa wa moto.