Wagonjwa waumia Kajiado mgomo ukiendelea kwa wiki ya tatu
MAMIA ya wagonjwa ambao wanategemea huduma katika hospitali za Kaunti ya Kajiado, wanaendelea kuumia kutokana na mgomo ambao umekuwa ukiendelea kwa wiki ya tatu sasa.
Zaidi ya wauguzi na wakunga 650 chini ya Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi na Wakunga (KNUNM) walianza mgomo wao Februari 28, 2025.
Hii ni baada ya kutoa notisi ya siku saba kwa serikali ya kaunti kuridhia matakwa yao lakini ikakosa kufanya hivyo.
Mgomo huo umesababishwa na kaunti kukosa kutekeleza makubaliano ya kurejea kazini yaliyoafikiwa Januari 16, 2025.
Makubaliano hayo yalisababisha kutamatishwa kwa mgomo ulioanza Desemba 18, 2024 kutokana na kutekelezwa kwa mkataba wa awali.
Wahudumu hao wanadai kuwa hawajakuwa wakipandishwa vyeo, makato yao ya pensheni hayajakuwa yakiwasilishwa kwa miezi 17 na pia ada ya matibabu haijakuwa ikiwasilishwa kwa Bima ya Afya ya Jamii (SHA).
Vilevile wahudumu hao wanataka kutekelezwa kwa mfumo mpya wa kiwango cha mshahara ulioafikiwa 2024 na pia wauguzi wengine zaidi kuajiriwa.
Waziri wa Leba Alfred Mutua alimteua Stanley Kemboi kuendeleza mazungumzo kati ya kaunti na muungano wa wauguzi lakini wawakilishi wa kaunti walikwepa mkutano huo.
Katibu Mkuu wa KNUNM Stephen Warutere alishutumu kaunti kwa kutumia vitisho dhidi ya wafanyakazi wanaogoma.
“Kaunti ya Kajiado ni mwajiri asiyetilia manani maslahi ya wafanyakazi. Baadhi ya wauguzi walipata barua za uhamisho, huku wengine wakitumiwa barua waeleze kwa nini wanashiriki mgomo,” akasema Bw Warutere.
“Hatutaingiwa na uoga, tutaelekea kortini kulinda wanachama wetu nasi tuko tayari kwa mazungumzo nyakati zote,” akaongeza.
Katibu wa KNUNM tawi la Kajiado Wilson Leala aliambia Taifa Dijitali kuwa alikuwa amepokea barua ya uhamisho hadi Shomple, Magadi, Kajiado Magharibi. Shampole ambayo ipo mashinani sana inapatikana kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania.
“Uhamisho huu unalenga kuninyamazisha kwa sababu kila mara kaunti inazozona na wanachama wetu, huwa nahamishwa lakini nitaendelea kuwatetea wanachama wetu,” akasema Bw Leala.
Katibu huyo alisema mgomo huo ulilemaza huduma za kimatibabu katika hospitali ya rufaa, hospitali nne za kaunti ndogo na zaidi ya zahanati 100.
Hospitali ya Kaunti ndogo ya Kitengela hata hivyo haijaathirika kwa kuwa bado inaendeleza huduma kwa kuwa ina wauguzi ambao huwa wameajiriwa kwa muda.
Chumba cha kujifungua kwa akina mama katika hospitali nacho kimelemewa kutokana na msongamano wa wanaofika kuhudumiwa.
Waziri wa Afya Kajiado Alex Kilowua alisema kaunti inaendelea na mashauriano ili huduma zirejelewe kama kawaida.
“Mgomo huu unawaumiza mamia ya wagonjwa lakini tumepiga hatua na tunakaribia kuelewana,” akasema Bw Kilowua.