Waiguru alia uharibifu Kirinyaga katika maandamano
GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru amekashifu vikali uharibifu, uporaji na mauaji ambayo yalishuhudiwa katika kaunti hiyo wakati wa Saba Saba.
Bi Waiguru alisema maandamano hayo yaliyokolea zaidi ukanda wa Mlima Kenya yamewaacha wengi wa wafanyabiashara wakiwa na hasara tupu.
Gavana huyo alisema ingawa hakuna nafasi ya polisi kuwaua na kuwateka nyara raia na maandamano yanastahili kuwa ya amani, raia nao wanastahili kuhakikisha wanapigania haki zao kwa njia ya amani.
“Jambo tuliloshuhudia lilikuwa ni uharibifu wa mali na biashara kuporwa Kirinyaga. Iwe maovu haya yalifanywa na wenyeji au wahuni kutoka nje, tunastahili kusaili tunaelekea wapi,” akasema Bi Waiguru kupitia taarifa akitaja vituo vya Wang’uru, Kagio, Sagana, Kerugoya, Kutus, na Kagumo kama vilivyoathirika zaidi.
“Kuchomwa kwa supamaketi na uharibifu wa mali unaharibu masuala ambayo yamekuwa yakipiganiwa na Gen Z.”
Hatufai kuwaruhusu wahuni waharibu biashara zetu,” akasema Bi Waiguru.
Kiongozi huyo alisema serikali inastahili kuwasikiza raia lakini pia akawataka wenyeji wajizuie kuharibu uchumi wa kaunti za Mlima Kenya ambao umejengwa kwa kipindi kirefu.
“Kwa nini wenyeji washiriki au watazame wengine wakiharibu biashara na ndugu na dada zao. Mbona tunaharibu msingi wetu wa kiuchumi?” akauliza.
Bi Waiguru alisema eneo la Mlima Kenya ndilo litapoteza zaidi iwapo uharibifu wa mali utaendelea kushuhudiwa wakati wa maandamano.