Wakazi wachemkia gavana kwa kuingilia biashara ya changarawe
BAADHI ya wakazi wa Kaunti ya Makueni na wahifadhi wa mazingira wamelalamikia hatua ya serikali ya kaunti hiyo kugeuza maeneo ya uchimbaji changarawe kuwa ya kibiashara.
Haya yamejiri huku uongozi wa Gavana Mutula Kilonzo Junior ukilenga ushuru wa Sh47 milioni kutoka kwa biashara hiyo kufadhili bajeti yake ya Sh11 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Makumi ya vijana hupata riziki katika maeneo ya mito na mabwawa wakichimba changarawe ambayo husafirisha Nairobi.
“Hatutaruhusu maeneo hayo yatumike kibiashara kwani wengi wanategemea maeneo hayo kupata riziki. Kando na hayo hatutaruhusu kitu kama hicho kuendelea hadi umma ushirikishwe na wakazi wa maeneo ya Kiimakiu/Kalanzoni Kata ya Kalanzoni waruhusiwe kutoa maoni yao,” ombi la baadhi ya wakazi wa eneo la Kiimakiu/Kalanzoni lililotiwa saini na David Kioko, Paul Mwololo, na Shadrack Nzioka, lilisema.
Mnamo Jumatano, Mamlaka ya Uhifadhi na Matumizi ya Changarawe Makueni, iliyopewa jukumu la kusimamia rasilimali hiyo, ilitangaza kuwa ilikuwa imefunga Mto Ndovoini katika Wadi ya Kiimakiu/Kalanzoni baada ya watu kumaliza bidhaa hiyo.
Mamlaka hiyo pia ilitishia kumfurusha mfanyabiashara wa changarawe aliyekabidhiwa Bwawa la Kilombo lililo katika kingo za eneobunge la Kaiti huku kukiwa na malalamishi kuwa wengi wanahusika katika biashara ya magendo.
“Kufuatia kikao kilichofanyika Agosti, 12, 2024, Mamlaka imefuta uchimbaji wa changarawe ndani na wa kibiashara katika Kata ya Tulimani na kuwaagiza wafanyabiashara wa bidhaa hiyo,” alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Bw Urbanus Ndunda.
Mmoja wa waathiriwa, Bw Alex Kiangi, alisema biashara hiyo inafanywa kwa kufuata sheria za uchimbaji wa changarawe zilizomo katika Sheria ya Uhifadhi na Matumizi ya changarawe Kaunti ya Makueni, 2015.
Hizi ni pamoja na kupiga marufuku uchimbaji na usafirishaji wa bidhaa hiyo usiku.