Habari za Kaunti

Wakazi waulaumu uongozi wa kaunti ya Nairobi baada ya makazi yao kuteketea

Na WINNIE ONYANDO March 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI ya Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja imenyooshewa kidole cha lawama kwa kutuma magari ya zima moto kuchelewa na bila maji ya kutosha mkasa unapotokea.

Ya hivi karibuni ni mkasa wa moto uliotokea eneo la Tassia jijini Nairobi ambapo wakazi wanalalamika kuwa magari ya zima moto yalifika kuchelewa na bila maji.

Baadhi ambao wamepoteza makazi yao wanasema kuwa hawangepata hasara kubwa ikiwa magari hayo yangefika kwa wakati na yakiwa na maji ya kutosha.

Mkasa huo uliotokea Machi 2, 2025 uliziacha zaidi ya familia 50 bila makazi.

Akizungumza na Taifa Dijitali, Nicholas Waweru, mmoja wa waathiriwa alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona mali yao ikiteketea kwa sababu gari la zima moto la kaunti halina maji ya kutosha kukabiliana na moto.

“Hii ni kama kuzembea kazini. Gari kama hilo kufika katika eneo la tukio na halina maji ni jambo la aibu na kushangaza mno,” alaisema Bw Waweru.

Kando na hayo, alitoa wito kwa gavana huyo kuwajibuka kwani kwani atawahitaji wananchi tena ifikapo 2027.

Mbunge wa wa Embakasi North, James Gakuya, ambaye aliongoza mchakato wa kugawa chakula, blanketi na godoro kwa waathiriwa, alimshutumu gavana Sakaja akisema kuwa anafaa kuwajibika.

“Gavana Sakaja hajaonekana katika eneo hili tangu mkasa huu ulipotokea Jumapili. Ni jambo la kushangaza kuwa serikali ya kaunti ina idara maalum inayotengewa pesa kukabiliana na mkasa wa dharura. Wako wapi wasimamizi wa idara hiyo,” alisema Bw Gakuya.

Naye diwani wa wadi wa Nairobi Kusini ambaye pia ni naibu kiongozi wa wachache katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, Waithera Chege ametoa wito kwa selikali ya kaunti kuimarisha huduma za dharura.

“Gavana anafaa kuwatumikia wananchi. Hajaonekana hapa ilhali hawa ndio walimchagua,” akaongeza Bi Chege.