Habari za Kaunti

Wanarika wanavyounganishwa na nafasi za ajira

Na WINNIE ONYANDO April 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAMPUNI ya Wave 360 Africa imezindua mpango wa kukuza vipaji vya wanafunzi wa vyuo vikuu na kuwaunganisha na mashirika ya kuajiri huku ikilenga kupanua soko lake na kufikia nchi jirani ya Uganda.

Kampuni hiyo pia itatoa mafunzo kwa wanavyuo nchini Uganda kuhusu umuhimu wa ‘kujiuza’ na kujenga uhusiano ili akihitimu mchakato wa kutafuta ajira usiwe mzigo.

Kwa utaalamu wa mikakati ya masoko ya “Below the Line” (BTL) na “Above the Line” (ATL), kampuni ya Wave 360 Africa inalenga kuunda mazingira jumuishi ya kibiashara yanayonuia kuleta uhusiano halisi na kuweka maslahi ya wanafunzi mbele.

Akizungumza na Taifa Dijitali Ijumaa Aprili 11, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Wave 360 Africa, Zedekiah Mukoya, alisisitiza kujitolea kwa kampuni hiyo katika kubuni, kuwasilisha, na kuendeleza mikakati inayowahamasisha na kuunda uzoefu wa kudumu miongoni mwa wanavyuo.

“Malengo yetu ni kujenga uhusiano wa kibiashara, kujenga vipaji, kuunda kizazi cha vijana kinachoweza kujitegemea, na kuongeza uelewa miongoni mwao. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, tumeweza kutembelea vyuo zaidi ya 30 na taasisi za TVET, tukiwafikia wanafunzi zaidi ya 100,000,” alisema Mukoya.

Pia alitoa wito kwa sekta binafsi na ya umma kuiga mfano wa Wave 360, unaolenga kuwapa vijana fursa za kujiinua hasa wa vyuo kupitia maonyesho ya talanta na biashara.

“Mbinu hii inaweza kuchochea uvumbuzi wa kisanii na kuleta suluhu ya kudumu kani vijana wetu wataweza kujitegemea,” akaongeza Bw Mukoya.