Habari za Kaunti

Wavuvi washauriwa kutumia vyema fidia ya Sh1.7b wakilipwa

April 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

WAVUVI walioathiriwa na ujenzi wa Bandari ya Lamu wameshauriwa kutumia vyema fidia watakazopokea kutoka kwa Serikali ya Kitaifa.

Hii ni kufuatia matumaini ya kupokea fidia hivi karibuni, baada ya hatua ya mwisho iliyosalia ya kutia sahihi mkataba wa malipo kutekelezwa na Gavana Issa Timamy.

Shughuli ya kutia saini mkataba huo iliandaliwa kwenye makao makuu ya kaunti ya Lamu mjini Mokowe Jumatatu, ili kuwezesha malipo hayo ya Sh1.76 bilioni kwa wavuvi waathiriwa.

Awali Bw Timamy alikuwa amedinda kuweka sahihi yake kwenye mkataba huo kwa madai kuwa orodha ilijumuisha majina ya watu wasiostahili kupokea fidia.

Mnamo Aprili, 2023, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilisitisha shughuli ya kutathmini majina ya wavuvi waliofaa kunufaika na mgao Huo wa Sh1.76 bilioni baada ya tetesi za ufisadi kukumba shughuli hiyo.

Baada ya uchunguzi kufanywa, ni wavuvi 4,102 kati ya 4,734 wa awali ambao EACC iliidhinisha.

Bw Timamy aliishukuru EACC kwa juhudi zake katika kuhakikisha wavuvi halali pekee ndio watakaopokea fedha za fidia.

Alisema utawala wake utaendelea kushirikiana na serikali kuu Na wawekezaji kuhakikisha miradi zaidi ya maendeleo inatekelezwa Lamu na pia wenyeji wananufaika.

“Furaha yangu ni kuona haki ikitendeka kwenye zoezi hili la fidia ya wavuvi,” akasema Bw Timamy.

Mwenyekiti wa Miungano ya Wavuvi (BMU) Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Somo, alielezea matumaini yake kwamba zoezi sasa litaharakishwa na wavuvi kupokea fedha zao.

“Tumeteseka muda mrefu baada ya maeneo yetu ya uvuvi kuharibiwa na ujenzi wa Lapsset. Hata hivyo tuna imani maisha yetu kama wavuvi yatabadilika hivi karibuni baada ya fidia kutolewa,” akasema Bw Somo.

Meneja Wa Ukanda wa Pwani wa Mradi wa Bandari ya Lamu na Miundomsingi ya Uchukuzi kati ya Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini (Lapsset), Bw Salim Bunu, aliwashauri wavuvi kuwa makini, hasa kimatumizi punde watakapopokea fedha hizo za fidia ili kuepuka ubadhirifu.

“Itakuwa ni hasara kwako kama mwenye kunufaika kutumia fedha Kwa njia ya ubadhirifu na kuishia fukara. Hizi ni fedha zinazofaa kukubadilishia maisha,” akasema Bw Bunu.

Mnamo Mei, 2018, Mahakama Kuu mjini Malindi iliamuru jumla ya wavuvi wa Lamu 4,734 kufidiwa kima cha Sh1.76 bilioni.

Hii ni baada ya mahakama kupata kuwa mradi wa bandari ya Lamu ni kweli ulisababisha athari kubwa, ikiwemo kuharibu maeneo ambayo tangu jadi yalikuwa yakitegemewa na wavuvi hao wa Lamu kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.