Habari za Kitaifa

Afisi za UDA Bondo zachafuliwa na wahuni

March 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA KASSIM ADINASI

VIJANA wenye hasira mnamo Jumatano walivamia jengo la afisi za UDA katika eneobunge la Bondo, Kaunti ya Siaya na kulipaka matope na uchafu.

Bondo ni nyumbani na ngome ya kisiasa ya kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga.

Afisi hizo zinapatikana Yimbo kwenye jengo lililokodishwa kisha likapakwa rangi na nembo za UDA. Zimekuwa zikitumika kuendeleza usajili wa wanachama wa UDA na mikutano ya mashinani ya maafisa wa chama hicho.

Tukio hilo limelaaniwa na baadhi ya wanasiasa wa UDA wakisema linaonyesha eneo hilo bado halizingatii demokrasia.

Aliyekuwa mwaniaji wa kiti cha Mwakilishi wa Kike wa Siaya Aber Dundee aliwataka wakazi wa eneo hilo wavumilie misimamo tofauti kisiasa. Bi Dundee ndiye alikodisha na kupaka rangi afisi hiyo.

“Hili ni jambo lisilokubalika kamwe kwa sababu muda wa siasa uliisha na hakuna anayeshughulika na hilo kwa sasa. Tunafaa kuruhusiwa kuweka mikakati yetu ya kisiasa bila kuingiliwa,” akasema Bi Dundee.

Pia alifichua kuwa alikuwa ameonywa na mwanasiasa mmoja wa kike kuhusu mipango yake ya kufungua afisi za UDA Bondo.

“Aliahidi kunionyesha kivumbi. Hii inamaanisha kuwa hatukubali maoni kinzani,” akaongeza.

Hili ni tukio la pili katika Kaunti ya Siaya ambapo afisi za UDA zinavamiwa baada ya nyingine kuchomwa mwaka 2023 wakati kulikuwa na maandamano ya Azimio nchini.

Bw Maurice Makorondo, aliyekuwa naibu meya wa manispaa ya Siaya kabla ya ujio wa ugatuzi, alishutumu kitendo cha kuvamiwa kwa afisi za UDA na kutoa wito kwa wakazi wavumilie vyama vingine kama ODM.

“Kwa zaidi ya miaka 30, ni watoto wetu hapa, baadhi wakiwa viongozi walipigania mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo, inasikitisha kuwa sasa wao na watu wetu ndio wanakataa vyama vingine,” akasema Bw Makorondo.

“Hata ODM ina afisi zake maeneo ambayo UDA ni maarufu. Tunakashifu tukio hili na tunaamini polisi wanaendeleza uchunguzi,” akaongeza.

ODM ina umaarufu Siaya na wakazi wa eneo hilo na maeneo mengine ya Nyanza wamekuwa wakionyesha utiifu wao kwa familia ya Odinga.

Hatua ya baadhi ya wanasiasa kufanya kazi na serikali baada ya uchaguzi wa 2022 ambao Bw Odinga aliupoteza, imewakasirisha wafuasi wa ODM.