Habari za Kitaifa

Afueni kwa wafanyakazi wastaafu serikali ikiingilia kati wapate pensheni zao

Na COLLINS OMULO November 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Kitaifa ameanzisha mpango wa kuondoa mvutano unaozingira deni la Sh85 bilioni ambazo wafanyakazi waliostaafu wanadai kutoka kwa serikali za kaunti.

Hatua hiyo huenda hatimaye ikachangia wastaafu hao kupokea pesa zao.

Waziri wa Fedha John Mbadi amebuni kamati wanachama 18 wanaoshirikisha wawakilishi kutoka asasi mbalimbali kupendekeza namna ya kulipa malimbikiza ya pesa hizo za pensheni.

Hatua iliyochukuliwa na Bw Mbadi inatokana na uamuzi wa Seneti kwamba Hazina ya Kitaifa ibuni kamati maalum ya kusaka njia za kulipa malimbikizi ya malipo ya pensheni.

Hii ni baada ya maseneta kupitisha ripoti iliyoandaliwa na Kamati ya Seneti kuhusu Uwekezaji na Hazina Maalum inayoongozwa na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi. Kamati hiyo imekuwa ikiendesha uchunguzi kuhusu mwenendo wa serikali za kaunti kutowasilisha malipo ya pensheni ya wafanyakazi wao kwa Hazina ya Kitaifa.

Mwaka jana, kamati hiyo ilikuwa imemwagiza aliyekuwa Waziri wa Fedha Professor Njuguna Ndung’u kubuni jopo kazi la kutatua mvutano kati ya mashirika ya pensheni na serikali za kaunti.

Jopokazi hilo lililalamika kuwa juhudi za kutatua mvutano huo hazijafaulu kwa sababu Msimamizi wa Bajeti amekataa kuidhinisha makubaliano ya kubadilisha madeni yaliyowekwa kati ya serikali za kaunti na mashirika ya pensheni hadi kibali kitolewe na Hazina ya Kitaifa.

Kibali hicho pia kinatarajiwa kutolewa na afisi ya Mwanasheria Mkuu.

Jopokazi hilo la kushughulikia kutowasilisha kwa makato ya pensheni na serikali za kaunti litaongozwa na mkuu wa kitengo cha Bajeti na Masuala ya Kiuchumi Albert Mwenda, kama mwenyekiti.

“Lengo la kuteuliwa kwa jopokazi hilo ni kutimiza lengo la serikali la kuhakikisha kuwa pesa za makato ya pensheni yanayowasilishwa na serikali za kaunti kwa wakati,” ikasema notisi iliyochapishw ana Bw Mbadi.

Kulingana na notisi hiyo iliyochapishwa Ijumaa wiki jana, wanachama wengine wa jopokazi hilo ni mkurugenzi wa idara ya pensheni Albert Kagika, Mkurugenzi wa Idara ya Kushirikisha Mahusiano kati ya Matawi ya Serikali Samuel Kiptorus na Bernice Mwangiu kutoka afisi ya Mwanasheria Mkuu.

Wengine ni Theodora Ochichi kutoka Afisi ya Msimamizi wa Bajeti, David Kitetu kutoka Kamati ya Kiufundi ya Kushirikisha Mahusiano ya Matawi ya Serikali na Moses Waitara kutoka Hazina ya Pensheni ya Serikali za Wilaya (Lapfund).

Wengine ni Jackson Nguthu kutoka Mamlaka ya Malipo ya Kustaafu (RBA), Austine Munene kutoka Baraza la Mabunge ya Kaunti, George Okioma kutoka Hazina ya Pensheni ya Serikali za Kaunti (CPF) Christopher Mitei, Isaac Koech kutoka CPF na Hillary Mwaita kutoka Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).

Pia kunao Beth Ndung’u kutoka Wizara ya Fedha, Joseph Eshiwani kutoka kitengo ya Huduma za Uhasibu katika Hazina ya Kitaifa, Michael Obonyo kutoka Idara ya Pensheni katika Hazina ya Kitaifa Joseph Mbatha na Carolyne Mage kutoka Baraza la Magavana (CoG).

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA