Afueni kwa Waititu korti ikikubali aombe dhamana upya
ALIYEKUWA Gavana wa Kaunti ya Kiambu, Ferdinand Waititu, amepata afueni baada ya Mahakama Kuu kumpa ruhusa ya kurekebisha ombi lake la kutaka kuachiliwa kwa dhamana akisubiri uamuzi wa rufaa yake dhidi ya kifungo chake cha miaka 12 jela kwa ufisadi.
Jaji Lucy Njuguna alisema kuwa ombi la Bw Waititu la kutaka kuwasilisha ombi mpya lina uzito na linastahili kusikizwa upya. Aliongeza kuwa ingawa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Bw Renson Ingonga alipinga, mahakama inaamini kuwa ni haki kumpa nafasi Waititu kuliko kukataa ombi hilo.
“Nimepitia rasimu ya rufaa( ya dhamana) na kwa maoni yangu, marekebisho yaliyopendekezwa ni muhimu kwa uamuzi wa haki wa rufaa hii,” alisema Jaji Njuguna.
Bw Waititu alihukumiwa kifungo cha miaka 12 mnamo Februari 14 kwa kupokea hongo ya Sh25.6 milioni kutoka kwa mkandarasi wa barabara alipokuwa gavana wa Kiambu. Aliagizwa kulipa faini ya Sh53.5 milioni kuepuka kifungo jela lakini hakuweza kulipa.
Hapo awali, ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana lilitupiliwa mbali na mahakama, ambayo ilisema kuwa rufaa hiyo itashughulikiwa kwa haraka. Mahakama pia ilikataa sababu za kiafya zilizotolewa, ikisema kuwa magereza yana huduma za afya zinazoweza kushughulikia matatizo ya kiafya ya Bw Waititu.
DPP alipinga ombi hilo jipya kwa madai kuwa halikuwasilishwa kwa kibali cha mahakama, na kwamba suala la dhamana lilikuwa tayari limeamuliwa. Hata hivyo, jaji alisema mahakama ina mamlaka ya kuruhusu marekebisho ya stakabadhi yoyote wakati wowote, mradi upande mwingine haupati madhara ambayo hayawezi kufidiwa kwa malipo.
“Mahakama inakubali ombi hili kwa kuwa lina mashiko,” alisema Jaji Njuguna, na kumuagiza Bw Waititu awasilishe rasmi rufaa hiyo ndani ya siku mbili kutoka tarehe ya uamuzi.