Aibu wanasiasa wakijivua ‘uheshimiwa’ kwa kupigana
WANASIASA sasa wanashiriki vitendo vya kujivua heshima huku wakitusiana na kupigana hadharani matukio ya aibu ambayo yamekashifiwa na raia na kupaka tope sifa zao.
Mnamo Jumanne, Aprili 8, 2025 Mbunge Maalum wa ODM Umi Harun na mwenzake wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Falhada Iman walipigana katika majengo ya bunge.
Mnamo Jumatatu, Aprili 7, 2025 madiwani wa Bunge la Kaunti ya Machakos walipigana, tukio ambalo lilisababisha diwani wa Matungulu Magharibi Raphael Nzau ajeruhiwe vibaya ndani ya bunge.
Bunge la Kaunti ya Nyamira nalo limekuwa likishuhudia mafarakano ya mara kwa mara na kwa sasa kuna mabunge mawili ya kaunti yanayoendeleza vikao vyake na yalianzishwa na mirengo miwili tofauti.
Sura ya sita ya Katiba inayozungumzia Uongozi na Maadili, inawatarajia watumishi wa umma, wawe na heshima na kujiepusha na vitendo ambavyo vitawasawiri vibaya machoni pa umma na nyadhifa wanazozishikilia.
Kwenye video ambayo kwa sasa imesambaa mitandaoni, Wakenya wamewakashifu Bi Umi na Bi Iman wakisema kitendo chao cha kupigana kwenye majengo ya bunge kilikuwa cha aibu na wanastahili wachukuliwe hatua kali.
Baadhi hata waliwakejeli kama waliopigana kizembe na kukashifu mlinzi wa bunge ambaye aliingilia kati kuwatenganisha, wakishauri wangeachwa walimane.
Bi Harun alisikitikia kupigana kwake na Bi Iman huku akisema amepiga ripoti kuhusu kisa hicho na kuomba msamaha kwa kitendo chenyewe.
“Nasikitikia kisa hiki kama mbunge na pia mama. Mwenzangu kutoka EALA ambaye amekuwa na tofauti kwa kipindi kirefu nami kutokana na kazi yangu, alionyesha tabia ambayo haifai kabisa,” akasema Bi Harun.
Kwa mujibu wa Sheria za Bunge, Bi Harun anastahili kuadhibiwa kwa kupigana katika majengo ya bunge.
Katika kisa cha Machakos, ilibidi spika wa bunge hilo Anne Kiusya kusitisha shughuli za bunge kuhakikisha usalama wake na wa madiwani.
Wakati wa purukushani hizo, madiwani walivunja samani na vifaa vingine vya bunge, huku mrengo mmoja ukipinga jaribio la kuwasilishwa kwa hoja ya kumwondoa kiongozi wa wachache Judas Ndawa mamlakani.
Bw Ndawa ni kati ya madiwani ambao wamekuwa wakitoa shinikizo kali ili Bi Kiusya aondolewe madarakani na baadhi ya madiwani walionekana kukerwa na hatua yake.
“Nzau alijeruhiwa wakati ambapo fujo zilizuka spika akijaribu kupenyeza hoja ambayo haikuwepo. Madiwani wameshikilia kuwa hakuna shughuli za bunge ambazo zitaendelea kama Bi Kiusya bado yupo mamlakani,” akasema Naibu Spika na diwani wa Ekalakala Stephen Mwanthi.
Bi Kiusya alijifungia afisini mwake siku hiyo yote huku madiwani wanaomuunga mkono nao wakidai anahujumiwa na wenzao wanaomshabikia Gavana Wavinya Ndeti.
Katika Kaunti ya Nyamira, kuna baadhi ya madiwani ambao wamekuwa wakihudhuria vikao vinavyoongozwa na Spika aliyetimuliwa Enock Okero huku mrengo mwingine ukiongozwa na Naibu Spika Thaddeus Nyaboro Nyabaro.
Kabla ya pande hizo mbili kutengana Novemba 2024, bunge la kaunti lilikuwa limegeuzwa uwanja wa makabiliano mara kwa mara.
Gavana Amos Nyaribo wiki moja iliyopita akiwa mbele ya Bunge la Seneti alisema kuwa anawazia kumshauri Rais William Ruto avunje kaunti hiyo kutokana na zogo la uongozi lisilokwisha.