Habari za Kitaifa

AMEMRUKA RUTO? Raila apiga abautani kuhusu mazungumzo, atoa masharti mapya

Na CHARLES WASONGA July 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga sasa amepiga abautani kuhusu mazungumzo ya kitaifa yanayopangwa na serikali kwa kutoa masharti kadhaa anayotaka yatimizwe kwanza.

Bw Odinga Jumapili alisema sharti haki itendeke kabla ya mazungumzo hayo yaliyoitishwa na Rais William Ruto kufanyika.

“Nakubaliana nanyi vijana kwamba haki ije kwanza kabla ya kuandaliwa kwa mazungumzo kwa sababu hiyo ni muhimu,” akasema kwenye taarifa.

Kulingana na kiongozi huyo wa Azimio, njia ya kupatikana kwa haki hiyo ni kwa serikali kuwafidia waathiriwa wote wa ukatili wa polisi na kesi zote dhidi ya wale waliokamatwa wakati wa maandamano ya Gen Z ziondolewe.

“Na polisi waliotenda unyama kama huo dhidi ya waandamanaji, wanahabari na Wakenya wengine wasio na hatia wakamatwe, washtakiwe na kufungwa jela,” Bw Odinga akaongeza.

Aidha, Bw Odinga anataka wale vijana waliotekwa nyara au wanaozuiliwa na polisi waachiliwe na matakwa ya wahudumu wa afya na walimu yatimizwe.

Vile vile, aliitaka serikali kusitisha utekelezaji wa Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF) na irejesha Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Afya.

“Baada ya masuala hayo kushughulikiwa, tunaweza kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa yatakayoendeshwa kwa uwazi mahala panapofaa kwa washiriki wote,” Bw Odinga akasema.

Alieleza mazungumzo hayo yashirikishe wawakilishi kutoka vijana, serikali, dini, wahudumu wa afya, mawakili, wanasiasa, walimu miongoni mwa nyanja nyinginezo.

“Na masuala yatakayojadiliwa yawe ni yale yanayohusu uongozi, kupanda kwa gharama ya maisha, vita dhidi ya ufisadi, vita dhidi ya ukabila, madeni ya serikali na usimamizi wa fedha za umma,” Bw Odinga akasema.

Siku chache zilizopita, kiongozi huyo wa Azimio aliunga mkono wito wa Rais Ruto kwamba kufanyike mazungumzo ya kujadili malalamishi yaliyoibuliwa na vijana wakati wa msururu wa maandamano yao kote nchini yaliyoanza Juni 18, 2024.

Bw Odinga aliunga mkono wazo hilo bila kuweka masharti yoyote, licha ya kupingwa na vinara wenzake katika Azimio na vijana hao wa kizazi cha Gen Z.

Wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, vinara hao wa Azimio pia walipinga wazo la kuundwa kwa serikali ya muungano wa kitaifa kwa kupitia uteuzi wa baadhi yao katika baraza jipya la mawaziri.

“Huu sio wakati wa mazungumzo; ni wakati wa kutekelezwa kwa matakwa yaliyoibuliwa na vijana wetu. Kama Azimio hatuwezi kushiriki katika mazungumzo kama hayo wala katika kuundwa kwa serikali ya muungano ilhali vijana wetu hawajatendewa haki,” Bw Musyoka akasema kwenye kikao na wanahabari katika SKM Centre, Nairobi.

Wengine waliopinga mazungumzo hayo na kushirikishwa kwa upinzani serikalini ni kiongozi wa chama cha DAP-Kenya Eugene Wamalwa, kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni miongoni mwa wengine.

Dakika chache kabla ya Rais Ruto kutaja baraza nusu la mawaziri Ijumaa, Bw Musyoka na wenzake walisema hawataunga mkono viongozi wa Azimio ambao huenda majina yao yalijumuishwa katika orodha ya mawaziri hao wapya.

“Wale kutoka Azimio ambao watakubali kuteuliwa katika baraza la mawaziri, wafahamu kuwa hawana baraka zetu. Watakuwa huko kama watu binafsi lakini sio kama wawakilishi wa Azimio,” akaeleza.