Habari za Kitaifa

Baada ya kutimua Riggy G, wabunge sasa waadimika vikaoni Spika Wetang’ula akinuna

Na DAVID MWERE October 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amesema wenyekiti wa kamati za bunge na manaibu wao ndio wanaoathiri zaidi majukumu ya Bunge la Kitaifa.

Alisema haya huku uongozi wa bunge ukipanga kuwachukulia hatua za kinidhamu wabunge kutatua tabia ya kususia vikao vya bunge ambayo imekithiri.

Mtindo wa wenyekiti wa kamati kukosa kuhudhuria vikao vya bunge na kamati ikiwemo kukosa kuwasilisha miswada na masuala mengineyo, kando na kuathiri shughuli za Bunge, imehujumu ajenda ya uongozi vilevile, alisema Spika.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah (Kikuyu), aliwaeleza wabunge, hususan wenyekiti wa kamati kupatia kipaumbele kuhudhuria vikao ili kuwezesha bunge kutimiza ajenda yake.

Kifungu 121 cha Katiba kinaagiza wabunge 50 kuwapo kabla ya kuanza kikao na 15 kwa Seneti.

Spika Wetang’ula alielezea kukata tamaa kutokana na mtindo wa kucheleweshwa kila mara miswada muhimu, hoja na malalamishi ya umma kwa sababu ya wabunge kutohudhuria.

Mnamo Oktoba 9, 2024, bunge lililazimika kuahirisha kikao cha asubuhi kwa kukosa idadi inayohitajika.