Bajeti: Omtatah kortini akilalamikia Seneti kurukwa
SENETA wa Busia Okiya Omtatah amewasilisha kesi katika Mahakama Kuu akidai Bunge la Seneti halishirikishwi katika maandalizi na uidhinishaji wa matumizi ya pesa zinazopitishwa katika Bajeti.
Bw Omtatah amesema Bajeti zinazopitishwa pasipo kushirikisha Bunge la Seneti hazina mashiko kisheria.
Seneta Omtatah amefafanua katika kesi hiyo kwamba Kifungu Nambari 39 (1) cha usimamizi wa matumizi ya pesa za umma (PFMA), kinakinzana na Katiba kwa vile kimeweka tarehe ya Juni 30 ya kila mwaka kuwa siku ya mwisho ya kuidhinishwa kwa mswada wa Fedha.
Pia, kifungu hicho kimeweka siku hiyo kuwa tamati ya kutiwa saini kwa hoja nyingine zote na Mswada wa Ugavi wa Pesa za Bajeti.
Seneta huyo amesema kutoshirikishwa kwa Seneti kwa Utengenezaji Bajeti na Ugavi wa Pesa kunainyima jukumu la kuhakikisha kuwa hakuna eneo humu nchini linalopuuzwa kwa njia yoyote ile katika ugavi wa pesa za kugharamia maendeleo.
Isitoshe, mwanasiasa huyo ambaye pia ni mwanaharakati anasema kushirikishwa kwa Seneti kunahakikisha kila kipengee katika hoja za Mswada wa Fedha kimeangaziwa ipasavyo.
Alisema lazima Bunge la Seneti lishirikishwe katika ugavi wa pesa kwa tume mbalimbali za kitaifa, huduma za pamoja za mabunge na afisi huru kulingana na Vifungu 96(1) na (2), 109 na 110 vya Katiba.
“Baada ya mapendekezo ya makadirio ya matumizi ya pesa kujadiliwa katika Bunge la Kitaifa, pia yanatakiwa kupelekwa katika Bunge la Seneti kujadiliwa tena na kupigwa msasa kabla ya kupelekewa Rais kuutia sahihi kuwa sheria,” Bw Omtatah anasema katika kesi aliyoshtaki kortini.
Jaji Lawrence Mugambi aliiratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru itajwe Julai 11, 2024 kwa maagizo zaidi.
Bw Omtatah amesema kutoshirikisha Bunge la Seneti katika utaratibu huo wa kuunda Bajeti kunaitia ndoa na dosari pamoja na kuhujumu Katiba.