Habari za Kitaifa

Bajeti ya 2024-25 itakomesha ukopaji, Waziri Kuria adai


WAZIRI wa Utumishi wa Umma, Moses Kuria, ameunga mkono bajeti mpya iliyosomwa Juni 13, 2024 na Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u akisema itawezesha Kenya kulipa madeni inayodaiwa na kukoma ukopaji.

Akisoma Makadirio ya Bajeti Mwaka wa Fedha 2024/25 mnamo Alhamisi, Waziri wa Fedha hata hivyo alisema ina pengo la Sh597 bilioni.

Waziri alifafanua kuwa pengo hilo litajazwa kupitia ukopaji kutoka mashirika ya humu nchini (Sh263 bilioni) na mataifa ya kigeni (Sh333 bilioni).

Akizungumza na Taifa Leo katika majengo ya Bunge baada ya Bajeti Mpya kusomwa, Waziri Kuria alipongeza bajeti hiyo akisema kando na kuwezesha Kenya kuishi kulingana na mapato yake, itaimarisha uchumi nchini.

“Tutaacha kukopa ili benki za humu nchini ziache kukopesha serikali pekee na kuanza kukopesha Wakenya vilevile. Benki zikifanya hivyo, uchumi utaanza kukua.”

Kulingana na Bw Kuria, ili kujaza pengo kwenye bajeti, “inamaanisha kwamba tutahitajika kuzalisha mapato yetu binafsi. Tutalazimika kutekeleza sera za kupunguza deni ili tuache matumizi ya fedha kiholela na kuacha kukopa.”

“Tupo kwenye mkondo sawa. Nina furaha na matumaini makuu kuhusu bajeti hii. Nina hakika kuwa katika muda wa miaka miwili ijayo, tutakuwa tumesawazisha bajeti yetu na tutaanza kuishi kulingana na uwezo wetu wa kimapato,” alisema.

Waziri alifafanua kwamba kwa muda mrefu, Kenya imekuwa iking’ang’ana tu kulipa malimbikizi ya deni.

Alisema serikali ya Rais William Ruto inapanga kufanyia mabadiliko mfumo wa deni ili kuufanya uwe na muda zaidi na usiolemea taifa.

Aidha, Bw Kuria alionekana kutetea serikali ya UDA kuhusu msururu wa ushuru uliopendekezwa katika Bajeti Mpya akisema kwamba Wakenya watavuna matunda hivi karibuni.

“Jambo la muhimu zaidi kuhusu bajeti hii ni kwamba, serikali inafanya uamuzi ufaao. Haifanyi maamuzi ya kujinufaisha kisiasa na kujivutia umaarufu. Tunafanya maamuzi mwafaka ambayo baada ya muda, Wakenya watajionea tulikuwa na nia njema.”

Huku akirejelea utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Waziri Kuria alitahadharisha kuhusu maamuzi yanayolenga kufurahisha umma.

“Katika serikali iliyopita, tulizidi kufanya maamuzi yaliyolenga tu kufurahisha watu, ili tushangiliwe na mambo yote kama hayo. Kinachonifanya nijivunie mno kuwa katika serikali hii ni kwamba tunafanya uamuzi unaofaa.”