Bei ya nyama yatarajiwa kupanda sikukuu ya Krismasi ikinukia
WAPENZI wa nyama huenda wakanunua bidhaa hiyo kwa bei ya juu msimu wa Krismasi mwaka huu kutokana na kupanda kwa bei ya mifugo katika Kaunti ya Kajiado.
Kwa miaka mingi, Kaunti hiyo imekuwa miongoni mwa wasambazaji wakubwa wa nyama, hasa katika miji midogo Nairobi na viunga vyake na huwezesha mapato ya Sh3.2 bilioni kila mwaka.
Hata hivyo, ukame mbaya wa 2020-2022 ulisababisha vifo vya mifugo 800,000 na kuacha familia 350 zikikabiliwa na njaa. Mvua ya hivi majuzi haijasaidia wafugaji wengi kurejesha mifugo wao.
Mfugaji kutoka Kajiado ya Kati Bw Stephen Nlabash, alisema licha ya kuwepo kwa malisho ya kutosha, wafugaji wengi hawako tayari kuuza mifugo wachache waliosalia baada ya ukame ulioshuhudiwa mwaka 2020-2022.
“Ni wafugaji wachache wanaomiliki mifugo wachache. Kwa sababu kuna malisho mengi, hawataki kuuza bali kuwanenepesha mifugo wakitarajia bei nzuri Januari,” alisema Bw Nkabash.
Katika masoko mengi ya mifugo, bei ya mbuzi au kondoo imepanda kutoka Sh8,000 mwaka jana hadi kati ya Sh15,000-20,000. Ng’ombe jike anauzwa kati ya Sh100,000 na Sh130,000, huku ng’ombe dume aliyekomaa akiuzwa kati ya Sh110,000 na Sh150,000.
Mwenyekiti wa Soko la Mifugo la Ilbisil, Bw James Ole Nkapapa, alisema bei za mifugo zitapanda zaidi siku ya Krismasi na hata kabla ya mwaka mpya.“Kuna uhaba wa mifugo, hasa ng’ombe, dhidi ya mahitaji makubwa kuelekea Krismasi. Tunatarajia bei za mifugo kupanda zaidi kati ya sasa na mwaka mpya,” alisema Bw Ole Nkapapa.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo katika vichinjio Kitengela Alhamisi asubuhi, ulionyesha upungufu wa mifugo. Vibanda vingi vilikuwa tupu, na shughuli zilikuwa chache ikilinganishwa na miaka ya nyumaMteja Bw James Ngumba, aliyetarajia kununua mbuzi watatu kwa Krismasi, alilazimika kununua mbuzi wawili tu baada ya bei kuongezeka.
“Nilikuwa na bajeti ya Sh30,000 kwa mbuzi watatu. Lakini nimewanunua wawili kwa Sh20,000 kila moja, sikuwa na chaguo lingine,” alisema.Bei ya jumla ya nyama kutoka vichinjioni imepanda kutoka Sh380 hadi Sh500 kwa kilo ya nyama ya ng’ombe, Sh550 hadi Sh700 kwa kilo ya nyama ya kondoo ikilinganishwa na mwaka jana.Wafanyabiashara wengi wanalazimika kutafuta ng’ombe kutoka Taita Taveta na Ukambani.
Katika maduka mengi Kitengela, kilo moja ya nyama ya ng’ombe inauzwa kati ya Sh580 na Sh600, huku nyama ya kondoo ikiuza kwa Sh800 kwa kilo kutoka Sh700 kwa kilo miezi michache iliyopita, hali inayowaudhi wapenzi wa nyama.