Kambi hasimu zajigawa ndani ya UDA ‘sawa na ilivyokuwa wakati wa Uhuruto’
WABUNGE wa UDA wameanza kujipanga kwenye mirengo ya Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua, pande zote zikionyeshana ubabe ndani ya chama hicho tawala.
Katika kile ambacho kinaweza kufananishwa na uhasama ulioshuhudiwa kati ya Rais Ruto na mtangulizi wake Rais Uhuru Kenyatta, Bw Gachagua mnamo Ijumaa alidai kuwa wanasiasa wanaoegemea mrengo wake wameanza kutishwa.
Kuibuka kwa kambi hizo mbili kulijitokeza wakati ambapo Bw Gachagua aliwaongoza wanasiasa wanaoegemea mrengo wake katika ibada ya kanisa kule Kasarani.
Wakati wa ibada hiyo Ijumaa iliyopita baadhi ya wandani wake walimshambulia Rais Ruto kuhusiana na nyongeza ya ushuru kwenye Mswada wa Fedha 2024.
Katika eneobunge la Gatundu Kaskazini, wabunge 18 wandani wa Rais Ruto nao waliendelea kumshambulia Bw Gachagua wakisema anasambaratisha utawala wa sasa ndani kwa ndani.
Vilevile kuibuka kwa kambi hizo mbili za kisiasa zilijitokeza wakati wa kupigia kura Mswada wa Fedha 2024 mnamo Alhamisi wiki jana.
Baadhi ya wabunge wandani wa Bw Gachagua walisusia kura hiyo au kupinga mswada wenyewe.
Mnamo Ijumaa, Bw Gachagua alidai kuwa baadhi ya wabunge wanaorindima ngoma yake wamekuwa wakitishwa na serikali.
“Ningependa kusema hapa leo kuwa safari ya kuunganisha Mlima Kenya imemalizika. Wananchi wote sasa wanazungumza kwa sauti moja,” akasema.
“Ni baadhi tu ya wanasiasa wachache hapa na pale. Baadhi wanatishwa, wanahangaishwa au kushurutishwa kwa kuambiwa kuwa wakizungumzia umoja wa mlimani basi maeneo yao hayatapewa miradi,” akaongeza.
Naibu Rais alisema kuwa wandani wake wanaambiwa kuwa wakionekana naye, basi mambo yatakuwa magumu kwao. Alikuwa ameandamana kwenye hafla hiyo na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, Seneta wa Kiambu Karung’o Thangwa na wabunge Simon King’ara (Ruiru), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), George Koimburi (Juja), Jayne Kihara (Naivasha), Wainaina Wambugu (Othaya), Onesmus Ngogoyo (Kajiado North), Wainaina Njoroge (Kieni) na Gathoni Wamuchomba (Githunguri).
Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na mawaziri wa zamani Eugene Wamalwa na Sicily Kariuki pia walikwepo. Magavana wa zamani wa Kiambu Ferdinand Waititu na James Nyoro na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Laikipia Cate Waruguru pia walihudhuria hafla hiyo.
Bw Koimburi ambaye ni kati ya wabunge wa UDA waliopiga kura ya LA kwa Mswada wa Fedha 2024, alisema hatatereka na anasimama na vijana ambao wanapinga mswada huo kutokana na kulimbikiziwa ushuru zaidi.
Mbunge huyo alisema kuwa mwaka jana aliunga mkono Mswada wa Fedha 2023 ambao uliweka makato ya nyumba lakini mwaka moja baadaye hakuna nyumba ambazo zimejengwa.
“Hapa Juja sijaona nyumba yoyote imekamilishwa na hata wiki kesho nitapinga mswada huo. Tutaendelea kumuunga mkono Naibu Rais kuunganisha Mlima Kenya,” akasema Bw Koimburi.
Wandani wengi wa Bw Gachagua Benjamin Gathiru (Embakasi ya Kati) Njeri Maina (Kirinyaga), Mohamed Ali (Nyali) na mbunge mteule wa Jubilee Sabina Chege hawakuwepo bungeni kupiga kura.