Habari za Kitaifa

DCI inavyolilia raia kuisaidia kumnyaka tena Collins Jumaisi

Na WYCLIFFE NYABERI August 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

IDARA ya Upelelzi wa Jinai (DCI), sasa inaomba usaidizi wa umma utakaosaidia kukamatwa tena kwa mshukiwa mkuu wa mauaji ya Kware, Collins Jumaisi Khalusha.

Jumaisi, pamoja na raia wengine 12 wa Eritrea, mnamo Jumanne, Agosti 20, 2024, walitoroka kutoka kituo cha polisi cha Gigiri walikokuwa wanazuiliwa.

Wa-Eritrea hao walikuwa wamekamatwa baada ya kuingia nchini kinyume cha sheria, ilhali Jumaisi alikamatwa baada ya wapelelezi kumhusisha na mauaji ya wanawake 42, ambao baadhi ya miili yao ilipatikana katika timbo la Kware, linalopatikana na Embakasi, jijini Nairobi.

Kufuatia kutoroka kwa 13 hao, kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli alisema kutoroka kwa Jumaisi na raia hao wa kigeni ilikuwa “kazi ya ndani.”

Bw Masengeli alidokeza kuwa uchunguzi wao wa mwanzo, uliashiria kuwa watoro hao walisaidiwa kukwepa rumande na baadhi ya maafisa wake waliokuwa kazini.

Kufuatia hayo, Bw Masengeli aliwasimamisha kazi kwa muda maafisa nane na tano kati yao, walifikishwa mahakamani mnamo Jumatano, Agosti 21, 2024.

Upande wa mashtaka uliomba kupewa muda zaidi kumaliza uchunguzi wao na uamuzi huo utatolewa leo Alhamisi Agosti 22, 2024.

Baada ya kujificha kwa siku mbili sasa, DCI katika mitandao yake ya kijamii, iliomba msaada wa umma utakaowasaidia kumnyaka tena Jumaisi.

“Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inatafuta usaidizi wa umma kutoa taarifa zinazoweza kusaidia katika kumkamata tena Collins Jumaisi Khalusha. Alikuwa anafaa kushtakiwa kwa mauaji lakini alikwepa mikononi mwa polisi mnamo Jumanne, Agosti 20, 2024,” ilisoma sehemu ya taarifa ya DCI.

Idara hiyo iliahidi kumtunuku kiasi cha pesa zisizojulikana yeyote atakayetoa taarifa zitakazowasaidia kumpata Jumaisi.

Kulingana na DCI, Jumaisi ni mzawa wa kata ndogo ya Shiru, kaunti ndogo ya Hamisi katika Kaunti ya Vihiga.

Walio na taarifa kumhusu, wametakiwa kupiga nambari ya wapelelezi 0800722203, 999, 911 na 112 au kutoa taarifa kwa kituo chochote cha polisi kilicho karibu.