Deborah Mlongo: Atoka kwa wagonjwa hadi kupanda miti
SIKU moja baada ya aliyekuwa Waziri wa Afya Deborah Mlongo Barasa kuhamishiwa Wizara ya Mazingira, Misitu na Mabadiliko ya Tabianchi, alianza kuchapa kazi kwa upanzi wa miti.
Dkt Barasa alianza kutekeleza rasmi majukumu yake mapya mnamo Alhamisi, Machi 27, 2025, baada ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Ruto Jumatano (Machi 26).
Aidha, Dkt Barasa alifungua jamvi la huduma eneo la Lelan, Kaunti ya Pokot Magharibi kwa kupanda miti.
Anachukua mahala pa Aden Duale ambaye ahamishwa hadi Wizara ya Afya.
Bw Duale sasa anatarajiwa kukabiliana na suala tata la utekelezaji mpango wa Afya kwa Wote (UHC) kupitia bima ya afya ya jamii (SHIF).
Dkt Barasa, ambaye ni daktari aliyebobea tiba ya magonjwa ya kuambukiza, alishukuru Rais Ruto kwa kumtwika wajibu wa kuongoza Wizara ya Mazingira.
Aliahidi kuendeleza mpango wa serikali unaoelenga kuhakikisha kuwa miti bilioni 15 imepandwa nchini kufikia mwaka wa 2032, akikariri umuhimu wa upanzi wa miti kama njia bora zaidi kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Upanzi wa miti husaidia sio tu kurejesha ubora katika ardhi iliyoharibiwa bali pia husaidia kujenga mustakabali mzuri kwa vizazi vijavyo,” akaeleza.
Dkt Barasa aliwataka Wakenya kupanda miti kwa wingi msimu huu wa mvua ya masika na kuitunza.
“Wanajamii wote wajitokeze kushiriki upanzi wa miti, kuanzia wanafunzi wa shule, familia na wakulima. Hii ndio njia ya kipekee ya kutunza mazingira yetu,” akaongeza.