Habari za Kitaifa

FKE yazimwa kuzungumza Leba Dei, Cotu na serikali zikishambulia waajiri

Na PETER MBURU May 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHIRIKISHO la Waajiri Kenya (FKE) Alhamisi Mei 1, 2025 lilizuiwa kuzungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi jijini Nairobi, huku Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu) ukiungana na serikali kulaumu waajiri.

Mkurugenzi Mkuu wa FKE Jacqueline Mugo, ambaye alikuwa amefika akiwa na hotuba yenye mapendekezo makali kwa serikali, hakupata fursa ya kuhutubu, huku Cotu ikishirikiana na serikali kuwashambulia waajiri.

Cha kushangaza ni kwamba, huku wafanyakazi wakiondoka mikono mitupu kwani Cotu na serikali hawakuwa na nyongeza ya mishahara, FKE ilikuwa na pendekezo yaliyolenga kunufaisha wafanyakazi.

Mapendekezo hayo yalijumuisha kuitaka serikali kupunguza ushuru wa nyumba nafuu hadi asilimia 0.5, kurekebisha viwango vya msamaha wa kodi hadi Sh36,000, na kutotoza ushuru bidhaa za chakula ili kupunguzia familia gharama ya maisha.

“Zaidi ya mishahara ya chini, tumependekeza mageuzi ili kuboresha ustawi wa wafanyakazi na kudumisha uendelevu wa biashara. Hii inajumuisha kutoza makato ya kisheria kwa mshahara wa msingi, kurekebisha viwango vya msamaha wa kodi kutoka Sh24,000 hadi Sh36,000, kupunguza ushuru wa nyumba nafuu hadi asilimia 0.5, na kutotoza ushuru bidhaa muhimu za chakula,” ilisema hotuba ya Bi Mugo ambayo haikusomwa.

FKE ilisema hatua hizo zingesaidia kupunguza gharama ya maisha kwa Wakenya, na hivyo kuongeza mapato yao na kufanya biashara za humu nchini kuwa na ushindani zaidi.

Waajiri pia walikuwa wamejiandaa kuomba serikali kutoa msimamo wake kuhusu mipngo yake ya kusaidia kampuni za humu nchini

“Serikali inapaswa kuwa na sera ya wazi ikiwa Kenya inalenga kuwa nchi ya uzalishaji au ya biashara. Tunatamani kuona Kenya kama nchi inayozalisha bidhaa na kuzisafirisha barani Afrika na duniani,” inasema hotuba ya Bi Mugo.

FKE pia ilikuwa na ombi kwa serikali kuhakikisha mazingira thabiti na yanayotabirika kwa biashara, pamoja na mfumo wa ushuru unaovutia uwekezaji ili kuunda ajira na kuongeza mishahara.

Shirikisho hilo lilikosoa viongozi wanaowataka vijana kujiajiri likisema wanakosa ukweli huku likisisitiza kuwa kuunda mazingira bora ya biashara kutasaidia kutatua tatizo la ukosefu wa ajira nchini.

“Wanasema vijana wanapaswa kujiajiri. Vijana wanapaswa kuunda ajira. Cha kusikitisha ni kwamba wote wanaoniambia haya wana ajira na wanapokea mshahara.

“Ikiwa sisi tunaopata mishahara hatuwezi kuwa na biashara, kujiajiri au kuunda ajira, basi ni vipi kijana maskini anayehitimu bila mtaji wowote atajiajiri? Lazima tuwe wa kweli,” ilisema hotuba ya Bi Mugo.