Ford Kenya kuunga mgombeaji wa UDA uchaguzi mdogo Malava, atangaza Wetang’ula
Spika wa Bunge la Kitaifa,Moses Wetang’ula, ametangaza kuwa chama cha Ford Kenya kitamuunga mkono mgombea wa chama cha UDA katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Malava unaotarajiwa hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa ibada ya kushukuru iliyofanyika kwa heshima ya Wakili Leonard Shimaka katika eneo la Lunyinya, Kaunti ya Kakamega, Spika Wetang’ula alisema kuwa Muungano wa Kenya Kwanza utamuunga mkono David Athman Ndakwa, mshindi wa mchujo wa UDA.
“Kama Ford Kenya, tumejitolea kuunga mkono mgombeaji wa Kenya Kwanza katika uchaguzi mdogo wa Malava, na tutakabiliana vikali na wagombeaji wengine kwa njia ya amani na ushindani wa haki,” alisema Wetang’ula.
Alihimiza umuhimu wa umoja miongoni mwa jamii na wagombea wote, akisisitiza haja ya kudumisha amani na mshikamano.
“Wagombea wote ni kama watoto wetu. Tunapaswa kushirikiana kuendeleza maendeleo ya eneo letu. Kiongozi wa kweli huweka mbele maslahi ya watu kuliko ya kibinafsi. Ni nadra kuona mgombea anayekubali kushindwa kwa heshima na kuendelea kusherehekea na wafuasi wake,” alieleza Wetang’ula.
Wetang’ula pia alitangaza kuwa ananuia kuwaunganisha wagombea wote waliopoteza kwenye mchujo ili kuwasilisha ujumbe mmoja wa umoja kwa wananchi wa Malava.
“Sisi ni Wakenya wapenda amani. Katika kila ushindani lazima kuwe na mshindi. Ni lazima tukubali kutofautiana bila kugombana na tuendelee mbele,” aliongeza.
Katika hotuba yake, Wetang’ula alieleza kuwa serikali inapanga kujenga na kukarabati barabara kutoka Misikoma, Sangalo, na Kambi hadi Lukume, kama sehemu ya mikakati ya maendeleo ya eneo hilo.
“Nimejitolea kujenga maabara ya kisasa ya kompyuta katika Shule ya Upili ya Mahira, na pia tutaleta umeme kwa jamii hiyo ili wanufaike moja kwa moja,” alisema.
Katika mchujo wa UDA, wagombea wanne walichuana kupata tiketi ya chama hicho, ambapo David Athman Ndakwa, MCA wa wadi ya Kabras Magharibi na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kaunti ya Kakamega, alishinda kwa kura 6,477. Ryan Malulu, mwanawe aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, alifuatia kwa kura 3,783.
Leonard Shimaka alipata kura 1,192 huku Simon Kangwana akifunga orodha kwa kura 1,064.
Malulu, ambaye alikuwa mfanyakazi wa zamani katika Tume ya Huduma za Bunge (PSC), alikuwa ameahidi kuendeleza urithi wa baba yake na kutekeleza ajenda za maendeleo kwa wananchi wa Malava.
“Ryan Malulu ni kama mwanangu. Nitamsihi arejee kazini kwake kwa sasa na aweke siasa pembeni hadi wakati mwingine,” alisema Wetang’ula.
Aidha, Spika Wetang’ula alionya kuwa mivutano ya ndani kati ya viongozi na jamii inaweza kudhoofisha maendeleo ya eneo la Magharibi.
“Tutashirikiana kwa pamoja kumpigia debe mgombea wetu. Tumekuwa na wagombea wazuri, na wote wana mustakabali mzuri kisiasa,” alisema.