• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
Furaha hatimaye msichana aliyeitwa shule ya wavulana kimakosa akitafutiwa sahihi

Furaha hatimaye msichana aliyeitwa shule ya wavulana kimakosa akitafutiwa sahihi

NA KASSIM ADINASI

Baada ya Taifa Leo kuangazia masaibu ya msichana mwerevu anayetoka familia maskini na aliyeitwa kujiunga na shule ya wavulana ya Lenana kimakosa, kuna matumaini baada ya Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti ndogo ya Siaya Maurice Saka na Naibu Kamishna wa Kaunti Robert Ng’etich kuingilia kati.

Wamempeleka mwanafunzi huyo, Gloria Adhiambo, aliyeathiriwa na mkanganyiko huo na wazazi wake katika shule ya wasichana ya kitaifa ya Ng’iya, huko Siaya.

Mwalimu Mkuu wa Ng’iya Hellen Owino anasema ametuma ombi ili kwamba Gloria awekwe katika shule yake badala ya Lenana.

“Tayari nimeweka ombi na kuna uwezekano mkubwa kwamba litakubaliwa. Utumaji wote wa wanafunzi katika shule za kitaifa hufanyika katika makao makuu ya Wizara ya Elimu, Nairobi,” alisema.

“Nina uhakika atapokea barua rasmi ya kujiunga na Ng’iya Girls hivi karibuni,” akaongeza.

Bw Saka alisema kwamba mkanganyiko huo ulitokea wakati wa shughuli ya usajili.

“Wakati aliposajiliwa, kulikuwa na makosa kuhusu jinsia. Badala ya kunakili kama mwanamke, ilinakiliwa kama mwanamume na hapo ndio mkanganyiko huo ulipotokea. Lakini tunamhakikishia Gloria na wazazi wake kwamba atatumwa katika shule ya kitaifa ambayo alifuzu kujiunga nayo,” akasema Bw Saka.

Soma hapa kuhusu kisa hicho kilivyoripotiwa: Msichana aitwa kujiunga na shule ya kitaifa ya wavulana

Maoni yake yanaungwa mkono na Bw Ngetich ambaye alisisitiza haja ya kuhakikisha anajiunga na shule ya kitaifa.

Kizingiti kikubwa kinachokodolea macho familia kwa sasa ni kupata karo inayohitajika kwa shule ya kitaifa.

“Binti yangu ni mwerevu na ana mustakabali mzuri. Lakini sina uwezo wa kifedha kugharamia karo na mahitaji mengine katika shule ya kitaifa atakayoitwa,” akahadithia babake Gloria, Bw Fredrick Owino.

Kinyume na awali ambapo alionekana kuzongwa na mawazo, uso wa Gloria mara hii uling’aa kwa furaha.

“Ng’iya ni shule nzuri na naomba nifaulu kujiunga nayo ili nitimize ndoto zangu,” akasema.

  • Imetafsiriwa na FATUMA BARIKI
  • Tags

You can share this post!

Ndindi Nyoro: Sasa sio mchele na nyama tu, tumeongeza...

Gavana Nassir atoa basari kwa wanafunzi wote wa kutwa...

T L