Habari za Kitaifa

Gachagua aapa atamenyana na Ruto 2027

Na  BENSON MATHEKA August 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, amethibitisha kuwa atawania urais mwaka 2027, akisema kuwa bado ana haki halali kisheria licha ya vuta nikuvute inayoendelea kuhusu kutimuliwa kwake ofisini.

Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja kupitia runinga ya Citizen, Agosti 26, 2025, kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) alisema kuwa Katiba ya Kenya inamlinda kuwania urais huku rufaa dhidi ya uamuzi wa kufurushwa kwake bado inaendelea.

“Nimehitimu na nina uungwaji mkono. Katiba inaruhusu mtu kuwania wadhifa wa kuchaguliwa hata kama amehukumiwa, iwapo bado hajatumia kikamilifu haki zake za kisheria. Mahakama ya Juu bado haijatoa uamuzi wa mwisho kuhusu kutimuliwa kwangu,” Gachagua alisema.

Mnamo Oktoba 2024, Bunge la Kitaifa lilipitisha hoja ya kumtimua kutoka kwa wadhifa wake, na Seneti ikaidhinisha kutimuliwa kwake kwa kupiga kura kwa misingi ya mashtaka matano kati ya kumi na moja yaliyowasilishwa. Mashtaka hayo yalihusu madai ya ufisadi, matumizi mabaya ya mamlaka, na kuchochea migawanyiko ya kikabila madai ambayo amekana mara kwa mara akisema ni kisasi cha kisiasa.

Baada ya kutimuliwa, Gachagua aliwasilisha kesi kadhaa mahakamani kupinga uhalali wa hatua hiyo na mchakato mzima wa bunge anaotaja kama wa kibaguzi na ambao haukufuata sheria.

Kwa mujibu wa Katiba, mtu anaweza kuwania wadhifa wa kuchaguliwa hata akiwa na kesi au rufaa inayoendelea, ikiwa hakuna uamuzi wa mwisho unaomfungia kuwania wadhifa huo. Huu ndio msingi wa hoja ya Gachagua: kwamba hakuna marufuku ya kudumu na hivyo yuko huru kugombea urais katika uchaguzi wa 2027.

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake Karen, Gachagua alizungumzia kwa mara ya kwanza kauli yake ya awali kuhusu “hisa serikalini,” akisema alikuwa chini ya shinikizo kutoka kwa jamii yake kuhakikisha Rais William Ruto anatimiza makubaliano yao ya kabla ya uchaguzi wa 2022.

“Serikali ya muungano huundwa kupitia makubaliano. Nilikaa na William Ruto kama mwakilishi wa watu wa Mlima Kenya na tukakubaliana kuwa atapokea asilimia 70 ya kura zetu kwa asilimia 40 ya nyadhifa serikalini,” alisema.

Alifichua kuwa ilikuwa ni makubaliano ya waungwana ambayo hayakuwekwa kwa maandishi. Alisema jamii za maeneo mengine kama Magharibi na Pwani zilijadiliana kwa makubaliano ya maandishi, jambo ambalo yeye hakufanya.

“Niliomba nafasi za baraza la mawaziri kama Wizara ya Mambo ya Ndani, Fedha, Kilimo, Ardhi, Biashara, Maji, Mwanasheria Mkuu na Maendeleo ya Miundombinu. Nilijadili pia kuhusu mageuzi ya kahawa na chai, na viwango vya chini vya malipo kwa wakulima,” alieleza.

Gachagua alisema matatizo kati yake na Rais Ruto yalianza pale Rais alipokataa kutekeleza kile walichokubaliana kabla ya uchaguzi.

Katika mahojiano hayo, Gachagua pia alijitetea dhidi ya tuhuma za kuwa mkabila, akisema kuwa ziara yake Amerika majuzi ilikuwa ya kitaifa na kwamba alikutana na Wakenya wote, ingawa baadhi ya mikutano iliandaliwa na jamii fulani kwa sababu ya masuala ya kipekee.

“Nilifanya mikutano ya hadhara iliyoshirikisha Wakenya wote, lakini pia nilihudhuria mikutano ya jumuiya mahususi zilizonialika. Hizi jumuiya hazikuanzishwa na mimi. Huko Amerika Wakamba wana chama chao, Waluo, Wamaasai, na jamii nyingine pia. Siwezi kukataa mwaliko kwa sababu tu umetoka kwa chama cha kabila moja,” alieleza.

Alisema kuwa lawama za ukabila ni propaganda kutoka kwa wandani wa Rais Ruto baada ya kutofautiana naye kisiasa.

“Wakati nilikuwa na Ruto, walikuwa wakinisifia kama mzalendo, mkakamavu, na kiongozi wa kitaifa. Lakini baada ya kutoka kwake, wakaanza kunitusi na kunipaka matope,” alisema.

Alisema kuwa yeye ni mzalendo anayependa jamii yake bila kuwachukia wengine.

“Mimi ni mzalendo. Napenda jamii yangu, lakini hiyo haimaanishi nawachukia wengine. Nataka mtu yeyote aniletee ushahidi wa video au sauti nikiwa nimetukana au kudhalilisha jamii nyingine yoyote,” alisema Gachagua.