Gachagua alengwa kwa vitoa machozi hafla ya maombi Nyandarua
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumamosi alilengwa kwa vitoa machozi wakati ambapo alihudhuria ibada ya makanisa mbalimbali katika bustani ya Shamata, Kaunti ya Nyandarua.
Gesi hiyo ya kutoa machozi iliyorushwa na mwanaume ambaye alikuwa amevalia nguo za raia, ilimlenga Bw Gachagua japo ilizuiwa na mmoja wa walinzi wake kabla ya kumfikia.
Walinzi wa Bw Gachagua kisha walimzingira na kumpeleka kwenye gari lake la kibinafsi ambalo lilikuwa umbali wa mita 10 kutoka mahali ambapo alikuwa ameketi.
Umati ulimvamia mwanaume aliyerusha gesi hiyo ya kutoa machozi wakampiga na kumjeruhi vibaya lakini akaokolewa na maafisa wa polisi.
Umma ulimwaandama mwanaume huyo hata baada ya polisi kumwokoa na ikawalazimu maafisa hao wa usalama watumie gesi za kutoa machozi na kufyatua risasi hewani kuwatawanya.
Raia waliwakashifu polisi wakidai walikuwa na ajenda fiche na walikuwa wakilenga kumdhuru Bw Gachagua ndiposa walimwokoa mwanaume huyo.
Tukio la kurushwa kwa vitoa machozi lilitokea baada ya Seneta wa Nyandarua John Methu kumaliza kuwahutubia raia na alikuwa karibu kuwaalika wengine wahutubu.
Baada ya ghasia hizo, raia walisema wameafikiana kuwa polisi hawafai kutoa ulinzi katika mikutano ya Bw Gachagua wakiahidi kuwa watamlinda wenyewe.
Maafikiano hayo yaliungwa mkono na viongozi wa kisiasa ambao walikuwa katika hafla hiyo. Mnamo Ijumaa jioni, waandalizi wa mkutano huo walikuwa wameshutumu serikali kwa kupanga kuuvuruga.
Walimlaumu Mbunge Mwakilishi wa Kike Faith Gitau na Mbunge wa eneo hilo George Gachagua wote ambao walikuwa wamepiga kura kuhakikisha kiongozi hiyo anabanduliwa kutoka wadhifa wake wa unaibu rais.
Akihutubu, Bw Gachagua alimlaumu Rais William Ruto kutokana na ghasia hizo akisema wale ambao wapo serikalini wanastahili kumakinika kutoa huduma kwa Wakenya badala ya kumlenga kisiasa.
“Rais anastahili kufahamu kwa nini Wakenya wana hasira na hawezi kuwalazimisha wampende. Tukio hili linaonyesha uoga na hawezi kuendelea kuwaumiza Wakenya kwa kuonyesha maoni yao katika mikutano ya umma,” akasema Bw Gachagua.
“Tulikuwa na Moi ambaye alikuwa dikteta na alienda nyumbani. Mbinu hizo zimepitwa na wakati na hazitafanya kazi katika enzi ya kisasa,” akaongeza.
Seneta Methu naye alisema Rais Ruto alikuwa amejaribu kuzima mkutano huo.
“Tunamwambia Rais kuwa unaweza kukataa kujenga barabara na kutunyima miradi lakini huwezi kutuzuia kukutana na kuandaa maombi,
“Lazima uheshimu makanisa na viongozi wa kidini wala hatutaingiwa na uoga na kutii amri yako ya kututishia kwa kutumia maafisa wa usalama,” akasema Seneta Methu.
“Hapa Mlima Kenya Gachagua ndiye kiongozi wetu na unastahili kuelewa hilo. Tutaendelea kumpenda na kuhudhuria mikutano yake,” akaongeza.