Gachagua amlilia Mungu viongozi wa Meru wakimhepa kanisani Meru
NAIBU Rais Rigathi Gachagua ambaye anakabiliwa na wimbi la kutimuliwa kwake afisini amewataka Wakenya wamwombee bosi wake Rais William Ruto na viongozi wengine ili kupunguza joto la kisiasa nchini.
Akiongea katika Kaunti ya Meru, Naibu Rais aliwataka viongozi ambao wana nia ya kumtimua wasubiri 2027 akisema kuwa hawawezi kubatilisha maoni ya Wakenya kwenye uchaguzi wa mnamo 2022.
“Endeleeni kuombea nchi, serikali, Rais na viongozi wote. Ni matumaini yangu kuwa joto la kisiasa litapuungua na wale ambao wanawavuruga wenzao wanastahili kumakinikia kuwahudumia Wakenya,” akasema Bw Gachagua.
Naibu Rais alikuwa akiongea katika eneo la Kinoru, Kaunti ya Meru baada ya kuhudhuria ibada kwenye Kanisa la Methodist.
“Tulichaguliwa miaka miwili iliyopita na sasa ni wakati wa kufanyia kazi Wakenya ambao walituchagua. Hatukupigiwa kura tupigane au kuraruana na kuangushana chini. Hilo ndilo ombi langu,” akaongeza.
Alionekana kumlenga Rais Ruto kwa kudai kuwa maamuzi ya watu yana uzito kuliko ya watu wachache wala hayafai kubatilishwa kwa kutumia njia nyingine.
“Uchaguzi ulifanyika na Rais na mimi tulichaguliwa kwa tikiti moja. Wakenya hawatafurahi iwapo mmoja ataondolewa ilhali walitupigia kura tukiwa wawili. Wanaoendelea kupanga njama ya kunitimua wasubiri baada ya miaka mitano,” akasema.
Alikuwa ameandamana na Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thang’wa, Joe Nyutu (Murang’a), Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga Njeri Maina, wabunge Peter Kihungi (Kangema), George Koimburi (Juja) na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Laikipia Cate Waruguru.
Hata hivyo, wanasiasa kutoka kaunti za Meru na Tharaka-Nithi walionekana kumwepuka Bw Gachagua wakati ambapo baadhi yao wanataka Bw Gachagua akitimuliwa, nafasi hiyo iendee Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki.