Gachagua arusha ‘mawe’ hafla ya kwanza tangu aponee uvamizi mazishini Limuru
ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumapili aliushambulia vikali utawala wa Rais William Ruto akiutaja kama usiokubali kauli na maoni pinzani.
Kwa mara ya kwanza, tangu nafasi yake ilipokabidhiwa rasmi Profesa Kithure Kindiki, Bw Gachagua alimsuta vikali bosi wake wa zamani kwa kutumia vitisho katika jaribio lake la kuwanyamazisha viongozi wenye kauli tofauti na wakosoaji wa utawala wake.
Vile vile, Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alisema serikali inaongozwa na nia mbaya inapochelewezesha kuanza kwa mchakato wa uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Akiongea wakati wa ibada katika kanisa moja eneo la Mwiki, eneo bunge la Kasarani, Kaunti ya Nairobi, Bw Gachagua alimtaka Rais Ruto kukoma kushambulia wakosoaji wa utawala wake baada ya kufaulu kunyamazisha Bunge na Idara ya Mahakama.
“Tunaitaka serikali ivumilie maoni na pinzani. Ikiwa Wakenya wanasema sera na mipango yako haifanyi kazi, usikasirike kwa sababu ni raia waliokuajiri na kama mabosi wako usikasirike wanapokuambia ukweli,” akasema Bw Gachagua.
Jana ilikuwa ni mara yake ya kwanza Bw Gachagua kuhudhuria shughuli ya hadhara baada ya kuponea kwa tundu la sindano, kundi la vijana walipotekeleza shambulio kali katika hafla ya mazishi aliyohudhuria eneo la Limuru, Kiambu.
Jana, Bw Gachagua alijitokeza kimasomaso kutetea kanisa. Alisema linashambuliwa na serikali kwa kuukosoa utawala na kuutaja kama unaozingatia uwongo, ukikosa kutimiza ahadi zake na kuendeleza vitendo vya ukiukaji wa haki za kibinadamu.
Bw Gachagua alisema kanisa ndiyo asasi ya kipekee iliyosalia na ambayo inaweza kutetea raia wa kawaida.
“Kwa hivyo, viongozi wanaoshikilia mamlaka za juu serikalini wanafaa kuwaheshima viongozi wa kanisa wanapotaja dosari katika serikali hii inayoshirikisha wanachama wa upinzani,” akaongeza
Bw Gachagua pia aliwataka viongozi wakuu serikalini na wanasiasa wandani wa Rais Ruto kukoma kushambulia kanisa.
Alisema viongozi wa makanisa hawajatenda kosa lolote wanaposema kuwa uchumi wa nchini haujaimarika na bima mpya ya afya na mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu imesheheni dosari nyingi zaidi.
“Hayo ndio ukweli, na viongozi wa mawaziri na wanasiasa marafiki wa rais hawafai kuwarushia cheche za maneno wanapoyataja,” akasema Bw Gachagua
Naibu huyo wa zamani wa rais alieleza kuwa viongozi wa makanisa ndiyo wanafahamu madhila yanayowasibu raia kwa sababu wao ndio hutangamana na Wakenya kwa ukaribu zaidi.
“Narudia kwamba viongozi wa kisiasa wanafaa kuheshimu Kanisa kwa sababu sauti ya kanisa ni sauti ya Mungu. Ilivyo sasa ni kwamba Wabunge wamenyamazishwa na ikiwa viongozi wa makanisa hawatatutea basi tutaisha kabisa,” akasema Bw Gachagua.
Juzi, wandani wa Rais Ruto wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Bunge Kimani Ichung’wa walitumia jukwaa la bunge kuwashambulia vikali viongozi wanaikosoa serikali huku wakifananisha hatua hiyo ni kujihusishwa kwao (viongozi wa kidini) katika siasa.
“Kuna mipaka kati ya siasa na dini. Kwa hivyo, wale viongozi wa kidini wanaojificha kwa kanisa na kwa upande mwingine wanaonekana kuchapa siasa ni wanafiki wakubwa zaidi,” Bw Ichung’wa akasema bunge wiki jana.
Lakini jana, Bw Gachagua alihimiza viongozi wa makanisa kuendelea kusimama na Wakenya.
“Endeleeni kusema ukweli na mtetee raia wanaokandamizwa na serikali hii dhalimu,” akasema.
Aliandamana na wabunge James Gakuya (Embakasi Kaskazini), John Kaguchia (Mukurweini), Wanjiku Muhia (Kipipiri), Jayne Kihara (Naivasha) na Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga Jane Njeri Maina.
Pia walikuwepo maseneta Joe Nyutu (Murang’a) na John Methu (Nyandarua).