Habari za Kitaifa

Gachagua ashambulia wanaopanga njama ya kumfurusha mamlakani

Na DANIEL OGETTA September 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU RAIS Rigathi Gachagua amewaonya wanasiasa wanaopanga kuwasilisha hoja ya kumtimua afisini kwamba hatishiki.

Akiongea Ijumaa, Septemba 20, 2024 alipowatembelea wafanyabiashara katika soko la mazao ya shambani la Marikiti, Nairobi, Bw Gachagua alisema yeye alichaguliwa na wananchi moja kwa moja na “siwezi kuondolewa afisini na watu wachache ambao wamenunuliwa.”

Serikali ya Kaunti ya Nairobi inataka kuhamisha wafanyabiashara hao hadi soko jipya la kisasa liliko kando ya barabara ya Kangundo, eneobunge la Embakasi Mashariki.

“Wale wanaopanga kuniondoa afisini nawaambia wathubutu. Ningependa kuwaonya dhidi ya kuniuzia uoga, ni Wakenya walionichagua walio na uwezo wa kunifuta kazi,” Bw Gachagua akaeleza.

Naibu Rais alisema hatatishwa kwa kusimama na Wakenya wenye mapato ya chini.

Bw Gachagua hakutaja watu wanaopanga njama ya kumwondoa afisini wala hatua ambayo wamepiga kufikia sasa.

Lakini alisisitiza kuwa njama hizo hazitafaulu.

Juzi, wabunge wandani wa Naibu Rais walidai kuna njama ya kumwondoa afisini ili kusambaratisha kampeni zake za kujenga umoja wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.

Walisema hayo siku chache baada ya angalau wabunge 50 kutangaza kuwa wanamtambua Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kama msemaji wao na kiunganishi kati yao na Rais William Ruto.

Bw Gachagua amekuwa akijinadi kama msemaji wa eneo la Mlima Kenya na mtetezi sugu wa maslahi ya wakazi wa eneo hilo.

Jijini Nairobi, Gavana Johnson Sakaja alitangaza wiki jana kwamba, serikali yake itawahamisha wafanyabiashara wa mboga na mazao mengi ya shambani kutoka soko la Marikiti ili kupunguza msongamano.

Lakini Gavana huyo alijibu malalamishi ya naibu rais akisema kuwa Bw Gachagua hafai kuwasiliana naye kupitia mitandao ya kijamii ilhali anayo nambari yake ya simu.

Ijumaa, Septemba 2024, 2024 Naibu Rais alirudia wito wake wa awali na kumtaka Gavana Sakaja kusitisha mpango wa kuwahamisha wafanyabiashara hao kutoka soko la Marikiti.