Gachagua atupwa nje ya serikali licha ya juhudi za kujitetea
NAIBU Rais Rigathi Gachagua ametimuliwa nje ya serikali licha ya juhudi kabambe za kujitetea dhidi ya mashtaka ya ukiukaji katiba yaliyowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Wabunge 281 kati ya 349 walipiga kura Jumanne jioni kumpiga teke naibu huyo wa Rais William Ruto, miaka miwili tu tangu asaidie kuunda ya Kenya Kwanza katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Mswada wa kumng’oa mamlakani uliwasilishwa wiki jana, baada ya tetesi za muda kwamba kulikuwa na njama za kumtimua mamlakani baada ya kile kilichoaminika kwamba ni kudorora kwa uhusiano kati yake na Rais Ruto.
Bw Mutuse aliwasilisha mashtaka 11 yaliyojumuisha ulimbikizaji wa mali ya Sh5.2 bilioni kupitia kwa ufisadi katika miaka miwili akiwa naibu rais pamoja na madai ya kugawanya Wakenya kupitia semi zake kuhusu ‘wenye hisa’ katika serikali ya Kenya Kwanza.