Habari za Kitaifa

Gachagua azidisha kasi ya ziara yake Amerika

Na Na David Monda  July 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua ameongeza kasi ya shughuli zake katika ziara yake Amerika, ambayo inalenga Wakenya waishio ughaibuni.

Kiongozi huyo wa chama cha DCP alianza ziara yake katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Amerika na jimbo la Washington. Jiji la Seattle lina maelfu ya Wakenya wanaovutiwa na hali yake ya hewa isiyo na baridi kali, ukaribu wake na Canada, kitovu cha utengenezaji wa ndege kupitia kampuni ya Boeing, na uchumi unaokua kwa teknolojia ya hali ya juu na ubunifu.

Kutoka Seattle, Bw Gachagua alielekea Washington DC, akazuru Boston, Massachusetts, na alitarajiwa kuwasili Maryland jana Jumamosi, Julai 26. Pia amepanga kutembelea majimbo ya Virginia, Pennsylvania na Delaware.

Umuhimu

Ziara hizi katika maeneo yenye idadi kubwa ya Wakenya inaonyesha umuhimu wa jumuiya ya raia wanaoishi ng’ambo, ambao huchangisha pesa kwa wagombeaji wa urais na pia huwasaidia kujijenga kisiasa mbele ya viongozi wa Amerika.

Kauli zake hadharani, mikutano ya kisiasa na maoni kutoka kwa waandalizi wa ziara na mikutano na wafuasi wake zinaonyesha kuwa kampeni ya Gachagua imelenga maeneo ya kimkakati yenye Wakenya wengi.

Kwa mfano, jiji la Baltimore katika jimbo la Maryland, ambapo alitarajiwa kutembelea jana, lina maelfu ya Wakenya na liko karibu na Washington DC – makao ya mamlaka ya Amerika.

Eneo hili la DMV (DC, Maryland, Virginia) linajitokeza kuwa nguzo muhimu ya kampeni ya Gachagua. Aidha, anawalenga Wakenya waishio Pennsylvania – hasa jijini Philadelphia – na jimbo la Delaware, ambalo pia lina idadi kubwa ya Wakenya.

Kulingana na Profesa David Kimori wa Chuo Kikuu cha Mankato State, Minnesota, ziara ya Bw Gachagua inalenga kuamsha uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya ughaibuni, hasa wale wenye mizizi ya Mlima Kenya.

“Wakenya wanaoishi ng’ambo wana ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya na katika kuchangisha fedha kwa wanasiasa. Pia huathiri sana familia na jamii zao wanazosaidia kifedha.

”Kwa upande wake, Profesa Eric Otenyo wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Arizona, alieleza matumaini kuwa tofauti na mwaka wa 2022, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itafanya kazi bora katika kuwasajili Wakenya wanaoishi Amerika kushiriki uchaguzi.

Hata hivyo, wakosoaji wa Bw Gachagua wanasema bado hajajivua nembo ya “kiongozi wa kikabila” na mtetezi wa jamii ya Mlima Kenya, hasa kutokana na kauli na mikutano yake.