Gachagua: Serikali inataka kunitilia sumu nife ndani ya miezi mitatu
ALIYEKUWA Naibu wa Rais Rigathi Gachagua Jumatatu alisema serikali ilitaka kumuua kwa kumwekea kemikali hatari ambayo ingemdhuru polepole kiakili na kumlemaza ndani ya miezi mitatu.
Bw Gachagua alikuwa mafichoni tangu taarifa kuzuka kuwa alikuwa akiandamwa na makachero kutoka Idara ya Upelelezi (DCI) Jumapili usiku.
Kiongozi huyo wa DCP jana alisema kuwa kuna kikosi maalum cha maafisa wa usalama ambacho kilikuwa kinamwandama ili kumtilia kemikali hatari jinsi alivyofanyiwa aliyekuwa kigogo wa siasa za upinzani marehemu Kenneth Matiba na uliokuwa utawala wa kidikteta wa Kanu.
Alisema kikosi hicho kinajumuisha maafisa wanaotoka DCI, Shirika la Ujasusi (NIS), kikosi cha Kupambana na Ghasia (GSU) na Polisi wa Utawala (AP).
“Tulipokea habari za kijasusi kutoka kwa polisi wazalendo ambao hawakuwa wamekubaliana na mpango wa kunidhuru kwamba waliamrishwa waweke bunduki na silaha kwenye msafara wetu. Huu ungekuwa ushahidi wa kutukamata na kutushtaki kortini,” akasema Bw Gachagua.
“Kikosi hicho cha mauaji kilijiunga na wenzao, ambao wamepewa mafunzo ya juu kuhusu kutumia silaha za kibayolojia (kemikali). Walikuwa wameamrishwa wanidhuru kwa kemikali ambayo ingelemaza akili zangu kwa muda wa miezi mitatu. Hili ndilo lilikuwa lengo la oparesheni yote,” akasema aliyekuwa naibu rais kwenye kikao na wanahabari nyumbani kwake kijijini Wamunyoro, Nyeri.
Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alidai kikosi ambacho kimekuwa kikimlenga kimekuwa kikishiriki mauaji na utekaji nyara ndiposa pamoja na wandani wake, walilazimika kubadilisha njia ambayo walikuwa wakifuata baada ya kubaini walikuwa wamewekewa mtego Murang’a.
Hata hivyo, alisema hajapiga ripoti kuhusu uvamizi huo kwa polisi kwa sababu ni maafisa hao hao wa usalama wanaotumiwa na serikali kumdhuru.
“Nitapiga vipi ripoti kwa watu wale wale ambao wanataka kunidhuru?”
“Ninazungumza hayo ili chochote kikinifanyikia, Rais William Ruto ndiye anastahili kuwajibika,” akasema.
Jana, Taifa Leo ilimfikia Msemaji wa Polisi Muchiri Nyaga ili kupata kauli yake kuhusu madai ya Bw Gachagua ila akasema hakuwa na lolote la kujibu.
“Kuhusu hilo hatuna la kusema,” akasema.
Aidha, juhudi za kupata maoni kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani ziligonga mwamba baada ya afisi ya Waziri Kipchumba Murkomen kutopokea simu.
Hata hivyo, wikendi, Bw Murkomen alisema kuwa hawatasita kumkamata Bw Gachagua hasa baada ya madai yake kwamba iwapo Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) itavuruga uchaguzi mkuu ujao, basi kutakuwa na ghasia mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa 2007.
“Wacha mwanaume huyo (Gachagua) aendelee kupiga kelele na kuwachochea Wakenya. Tutamkamata,” akasema Bw Murkomen akiwa Iten, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Alirudia matamshi hayo akiwa Kaunti ya Trans Nzoia akisema Bw Gachagua “hayuko juu ya sheria” na serikali itawaandama viongozi ambao wanawachochea raia na kuiharibia serikali sifa.
“Wajue kwamba wataguswa. Tumemakinika kuhakikisha kuna amani na usalama wa taifa hili wala hatutatishwa na yeyote akifikiria tutamwacha kwa sababu ya nafasi yake,” akaongeza.
Akijitetea, Bw Gachagua alisema kauli yake ilikuwa ikilenga kuwahamisisha Wakenya ikizingatiwa ghasia za baada ya uchaguzi zimesababisha maisha kupotea mnamo 1992, 1997 na hata kura tata ya 2007.
Alitaja kisa ambacho watu walichomwa kwenye kanisa eneo la Kiambaa, Kaunti ya Uasin Gishu baada ya uchaguzi wa 2007 kama mojawapo ya matukio mabaya zaidi nchini yanayostahili kuwa funzo.
Jana, alisema kuwa haogopi kukamatwa na yuko tayari kutoa majibu iwapo serikali inafahamu kuwa amefanya kosa lolote.
“Wanajua maboma yangu yote na niko hapa, hawahitajiki kunikujia barabarani. Waje tu hapa na kama nimefanya uhalifu wanikamate na kuchukua hatua zozote wanazotaka,” akasema.
Pia alizungumzia mpango wa kuhakikisha kuwa walinzi wake wa kibinafsi ambao wanamiliki bunduki kwa njia halali wanapokonywa silaha ili adhuriwe.
Alisema Rais Ruto amekerwa na idara ya usalama hasa baada ya walinzi hao kutibua majaribio mengi ya kumdhuru.
Alitaja visa mbalimbali ambapo maisha yake yamelengwa lakini hadi leo hakuna aliyekamatwa au kuchukuliwa hatua kali za kisheria.